Mwili wa mwanawe mbunge David Sankok kufanyiwa uchunguzi upya

Muhtasari

• Jopo la wachunguzi liliundwa upya ili kuwawezesha kujibu maswali mengi ambayo hayajajibiwa, kupata historia ya risasi ya muuaji na kukusanya ushahidi zaidi. 

• Shughuli ya uchunguzi wa maiti hiyo zitafanyika mjini Nakuru.

• Mwanapatholojia mkuu wa Serikali Johansen Oduor ataongoza zoezi hilo mjini Nakuru.

Mbunge maalum David Sankok akiwa bungeni
Mbunge maalum David Sankok akiwa bungeni
Image: MAKTABA

Mwili wa Memusi Sankok, 15, ambaye ni mtoto wa mbunge maalum David Sankok na ambaye inasemekana alijipiga risasi na kujiua nyumbani kwa babake Mei 2, utafanyiwa uchunguzi wa pili leo (Ijumaa). 

Shughuli ya uchunguzi wa maiti hiyo zitafanyika mjini Nakuru ambako mwili huo unahifadhiwa na itakuwa sehemu ya mchakato wa kukusanya ushahidi baada ya kubainika kwamba uchunguzi wa awali ulifanywa na afisa wa Wizara ya Afya bila kushirikisha wataalam wa uchunguzi na hivyo kukosa kutoa majibu muhimu. 

Mwanapatholojia mkuu wa Serikali Johansen Oduor ataongoza zoezi hilo mjini Nakuru ambapo mwili huo ulihamishwa kutoka katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Longisa, Kaunti ya Bomet. Uchunguzi wa awali wa maiti ulionyesha kuwa kifo cha Memusi kilisababishwa na risasi kwenye kidevu chake na kutokea juu ya kichwa chake. 

Uchunguzi wa kitaalamu uliopangwa utahusisha kuchunguza jeraha lililosababishwa na risasi ili kubaini ikiwa linaendana na kusababishwa na risasi hiyo, mwelekeo ambao risasi ilichukua na hata ganda ambalo linaweza kuhusisha matumizi ya X-ray. 

Kikosi cha wapelelezi kutoka Kitengo cha Mauaji katika idara ya DCI Kilichukua jukumu la uchunguzi wa kifo cha mvulana huyo katika Kaunti ya Narok. 

Jopo la wachunguzi liliundwa upya ili kuwawezesha kujibu maswali mengi ambayo hayajajibiwa, kupata historia ya risasi ya muuaji na kukusanya ushahidi zaidi. 

Walisema ziara hiyo ambayo sasa ni ya nne katika eneo la tukio ilikuwa ni sehemu ya ukusanyaji wa ushahidi.