Mshtuko baada ya mwanaume kuua bintiye kisha kujitoa uhai Kirinyaga

Muhtasari

• Mwanamume huyo anasemekana kuenda na bintiye kujiburudisha katika  baa moja ya eneo hilo ambapo anadaiwa kumpatia sumu.

•Alikuwa ametengana na mama ya msichana huyo kutokana na matatizo ya nyumbani na aliishi na bintiye katika mji wa Wang'oru.

Mshtuko baada ya mwanaume kuua bintiye kisha kujitoa uhai Kirinyaga
Mshtuko baada ya mwanaume kuua bintiye kisha kujitoa uhai Kirinyaga
Image: WANGECHI WANG'ONDU

Hofu ilitanda katika kijiji cha Piai, eneo la Mwea, kaunti ya Kirinyaga baada ya wakazi kuamka Jumamosi na kupokea habari za kusikitisha za mwanamume anayeshukiwa kumuua bintiye kabla ya kujitoa uhai.

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 30 anasemekana kuenda na bintiye kujiburudisha katika  baa moja ya eneo hilo ambapo anadaiwa kumpatia sumu.

Baada ya  kumuua binti yake, mwanamume huyo anadaiwa kubugia chupa nyingi za pombe kali na baadaye kujitoa uhai kwa kujinyonga.

Mwili wake ulikuwa wa kwanza kugunduliwa na wafanyikazi katika baa hiyo. Baada ya hapo binti  yake alikutwa chumbani akiwa amekufa.

Mkuu wa polisi wa eneo la Mwea Daniel Kitavi alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa kulikuwa na chupa ndogo ya sumu ambayo iligunduliwa ndani ya chumba inayodaiwa huenda ilitumika kumuua msichana huyo. 

Kitavi alificha majina ya waathiriwa kwani familia bado haikuwa imefahamishwa kuhusu tukio hilo. 

Alisema polisi bado hawajabaini kilichomsukuma mwanaume huyo kufanya kitendo hicho. 

Bosi huyo wa polisi alifichua kuwa mwanamume huyo alikuwa bado alikuwa mlevi wakati  alipofanya kitendo hicho. 

Mwanaume huyo alikuwa ametengana na mama ya msichana huyo kutokana na matatizo ya nyumbani na aliishi na bintiye katika mji wa Wang'oru.

“Uchunguzi unaendelea kubaini kilichosababisha afanye kitendo hicho cha kinyama,” alisema.

Miili hiyo ilepelekwa katika hospitali ya rufaa ya Kerugoya ikisubiri uchunguzi wa maiti.

(Utafsiri: Samuel Maina)