Afueni huku ushuru kwa gesi ya kupikia ukipunzwa hadi 8% kutoka 16%

Muhtasari

• Unga wa mihogo, mahindi na ngano utasalia katika kitengo cha bidhaa ambazo hazitozwi ushuru na bidhaa hizo hazitatozwa ushuru wa thamani ya bidhaa.

Ni afueni kwa wananchi wanaotumia gesi ya kupikia baada ya bunge kupunguza ushuru wa thamani ya bidhaa kwa bei ya gesi kutoka asilimia 16 hadi asilimia nane.

Mabadiliko haya yaliidhinishwa katika mswada wa kifedha uliyopitishwa bungeni siku ya Alhamisi jioni na sasa yanasubiri tu idhinisho la rais Uhuru Kenyatta atakapoweka saini yake.

Ni habari njema pia kwa sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa la Kenya kwani mswada huo uliopitishwa pia uliondoa ushuru unaotozwa mbolea, hatua ambayo inatarajiwakupunguza kwa bei ya mbolea kwa kiasi kikubwa.

Kwa muda sasa wakulima wamekuwa wakilalamikia bei ghali za mbolea na pembejeo hali ambayo imefanya gharama za ukulima kuwa juu.

Katika mswada huo ushuru unaotozwa huduma za dijitali utasalia asilimia 1.5.

Unga wa mihogo, mahindi na ngano utasalia katika kitengo cha bidhaa ambazo hazitozwi ushuru na bidhaa hizo hazitatozwa ushuru wa thamani ya bidhaa.

Ushuru unaotozwa pombe aina ya KEG utasalia shilingi 121.85 kwa lita huku ushuru unaotozwa vinywaji ambavyo sio pombe ukisalia shilingi 6.03 kwa lita moja.

 Wapenzi wa vileo hata hivyo watagharamika zaidi baada ya ushuru kuongeza kwa vileo mbali mbali.

Ikiwa mswada wa kifedha utatiwa saini na rais Uhuru Kenyatta basi bia zote zenye kiwango cha cha pombe cha zaidi ya asilimia sita zitatozwa ushuru wa shilingi 134 kwa kila lita kutoka shilingi 121.85.

Mvinyo (wine) utatozwa ushuru wa shilingi 229 kwa kila lita kutoka shilingi 208.20.

Pombe kali za kiwango cha pombe cha zaidi ya asilimia sita sasa zitatozwa ushuru wa hadi shilingi 335.30 kutoka ushuru wa awali wa shilingi 278.70 kwa lita moja.

Ushuru unaotozwa ada za matangazo ya biashara ya pombe, kamari na kuwekeana dau kwenye mageziti, televisheni, mabango na vituo vya radio yatatozwa ushuru wa asilimia 20.

Mayai yanayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa minajili ya kuzalisha kuku yameondolewa kutoka orodha ya bidhaa za kutozwa ushuru.

Bunge liliongeza muda wa vikao vyake siku ya Alhamisi ili kujadili mswada huo muhimu hadi usiku, kikao hicho hata hivyo kulihudhuriwa na wabunge wachache huku wengi wao wakisalia katika maeneo bunge yao wakifanya kampeini kwa uchaguzi mkuu ujao.