Kalonzo ajiondoa rasmi kutoka kinyang'anyiro cha urais

Muhtasari

• Kujiondoa kwake rasmi katika kinyang'anyiro cha Urais kunakuja siku moja tu baada ya Kalonzo kutangaza kumuunga mkono mgombeaji wa muungano wa Azimio - OKA Raila Odinga.

Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amejiondoa rasmi kutoka kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Ijumaa, Kalonzo alisema hatawasilisha stakabadhi zake kwa tume ya uchaguzi na mipaka IEBC mnamo Juni 4 kama ilivyopangwa awali.

Kujiondoa kwake rasmi katika kinyang'anyiro cha Urais kunakuja siku moja tu baada ya Kalonzo kutangaza kumuunga mkono mgombeaji wa muungano wa Azimio - OKA Raila Odinga.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wanachama wa muungano huo siku ya Alhamisi, Kalonzo alisema alichukua uamuzi huo kuzima azma yake kwa muda kwa ajili ya nchi.

Kalonzo siku ya Alhamisi akitangaza kuungana tena muungano wa Azimio Kalonzo vile vile pia alikubali nafasi ya waziri mkuu ambayo alipewa katika muundo wa serikali ya Azimio-OKA.

“Nimeamua kukubali kwa unyenyekevu na kuthamini kuteuliwa kwangu kama Waziri Mkuu katika muungano wa Azimio,” Klonzo alikariri.  

Kujiondoa rasmi kwa Kalonzo kwenye kinyang'anyiro hicho kunamaanisha kuwa hatafika mbele ya tume ya uchaguzi katika mchujo unaoendelea wa wagombea Urais.

Makamu huyo rais wa zamani alisema kwamba ni wazi kuwa muungano wa Azimio–OKA utaunda serikali.