Mwanadada afariki baada ya kuanguka kutoka kwa ghorofa wakati akipigana na mpenziwe

Muhtasari

•Polisi wamesema wanamsaka Peter Kamau Kuria mwenye umri wa miaka 32 kufuatia kifo cha mpenzi wake mwenye umri wa miaka 25. 

•Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya kufanyiwa utambuzi na uchunguzi.

crime scene
crime scene

Mwanamume mmoja anayedaiwa kumsukuma mpenzi wake kutoka ghorofa ya tano katika eneo la Drive Inn Nairobi yuko mbioni.

Polisi wamesema wanamsaka Peter Kamau Kuria mwenye umri wa miaka 32 kufuatia kifo cha mpenzi wake mwenye umri wa miaka 25. 

Mwanamke huyo alikuwa amemtembelea Kuria nyumbani kwake Alhamisi asubuhi kabla ya mzozo kusikika kutoka kwa nyumba hiyo.

Wapangaji wa nyumba hiyo waliwaambia polisi kwamba walisikia kishindo kwenye ghorofa ya chini na walipoangalia wakaona mwili wa mwanamke ukiwa umezingirwa na damu nyingi. 

Mwanamke huyo alifariki papo hapo katika eneo la tukio huku fuvu la kichwachake likipasuka kufuatia kisa hicho kilichotokea mwendo wa saa nane usiku wa kuamkia Alhamisi.

Polisi waliitwa kwenye eneo la tukio na wakabaini kuwa Kuria hayupo kwenye nyumba yake ambayo ilikuwa imefungwa.

Walinzi wa ghorofa hiyo ni miongoni mwa waliohojiwa kuhusu tukio hilo.Mkuu wa polisi wa Nairobi James Mugera alisema wanamsaka Kamau kwa ajili ya mahojiano.

"Hatujui ni nini kilijiri lakini tunamtafuta mshukiwa ili atupatie habari zaidi," alisema.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya kufanyiwa utambuzi na uchunguzi.

Katika eneo la Embakasi, mvulana wa umri wa miaka 11 alivunjika taya, mikono yote miwili na mguu wa kulia baada ya kuruka kutoka ghorofa ya tatu ya shule yao baada ya kuadhibiwa na wasimamizi wa taasisi hiyo.  

Polisi walisema kuwa waliarifiwa mvulana huyo alikuwa hospitalini baada ya kuruka katika jaribio la kujitoa uhai baada ya kuadhibiwa kwa utoro.

Polisi walisema wanachunguza tukio hilo. 

Na polisi wanamsaka mtu mwenye bunduki ambaye alimpiga risasi kondakta na kumjeruhi vibaya  katika eneo la Allsops. 

Inasemekana kuwa mshambuliaji huyo alitoroka mara baada ya tukio hilo la saa mbili usiku na sababu bado haijafahamika. 

Kondakta huyo alijeruhiwa mkononi. Hii ilikuwa ni baada ya risasi  kupenya kwenye kioo cha mbele na kumpata akiwa ameketi  kwenye siti ya nyuma.

Alikimbizwa hospitalini ambako alihudumiwa huku msako mkali ukianzishwa kumtafuta aliyefyatua risasi.

Risasi mbili zilizotumika zilipatikana katika eneo la tukio na kuchukuliwa kwa uchambuzi wa ballistic. 

Kwingineko, mshukiwa wau jambazi alipigwa risasi jana usiku na kuuawa katika eneo la South B jijini Nairobi na bastola kupatikana juu yake. 

Polisi wanasema mwanamume huyo alikuwa akiendesha pikipiki na alifukuzwa kwa muda mrefu baada ya kufanya wizi katika eneo la Viwanda jijini. 

Mshirika wake alifanikiwa kutoroka kisa hicho na polisi wanasema wanamtafuta. Visa vya unyang’anyi wa kutumia silaha vimekuwa vikiongezeka jijini na kusababisha polisi kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo. 

Mugera alisema wametuma wafanyikazi zaidi kushughulikia kesi hizo.