DCI yamsaka jamaa anayedaiwa kuvamia maduka ya Mpesa na kuua maajenti wa wawili

Muhtasari

•Inaripotiwa kuwa genge hilo limekuwa likitekeleza wizi katika maduka ya Mpesa waliyolenga huku wakiwa wamejihami kwa silaha hatari.

•Mkuu wa DCI amewaomba Wakenya watakaotambua sura ya jamaa huyo kutoa ripoti ili kufanikisha  kukamatwa kwao.

Image: FACEBOOK// DCI

Wapelelezi wa makosa ya jinai wanasaka genge la majambazi ambao wamekuwa wakivamia maduka ya Mpesa jijini Nairobi na viunga vyake.

Inaripotiwa kuwa genge hilo limekuwa likitekeleza wizi katika maduka ya Mpesa waliyolenga huku wakiwa wamejihami kwa silaha hatari.

Majambazi hao hatari wanaripotiwa kuwaua maajenti wawili, mmoja wa kike na mwingine wa kiume, katika eneo la Adams Arcade siku ya Jumamosi.

Alhamisi asubuhi mkuu wa DCI aliachia sura ya mmoja wa majambazi hao ambaye alinaswa na kamera za CCTV katika duka moja walilovamiwa.

Aliwaomba Wakenya watakaotambua sura ya jamaa huyo kutoa ripoti ili kufanikisha  kukamatwa kwao.

"Tunaomba utusaidie katika kumtafuta mshukiwa na kutoa haki kwa familia za marehemu na maajenti wengine wengi wa Mpesa wanaoendelea kuteseka mikononi mwao," Taarifa ya DCI ilisoma.

Kinoti pia ameachia video inayoonyesha mshukiwa akitekeleza wizi katika duka moja ya maduka ya Mpesa jijini Nairobi.

Katika video hiyo, mshukiwa anaonekana akizungumza na mhudumu wa Mpesa wa kike huku akiendelea kuhesabu noti za pesa.

Baada ya kubadilishana maneno yasiyosikika kwa sekunde chache, mshukiwa anaonekana akinyakua simu kutoka kwa dirisha ya duka hilo.  

Mhudumu huyo wa Mpesa anaonekana akilalamika kuhusu kitendo hicho ila mshukiwa ananyakua virago vyake na kuondoka.

Kitengo cha DCI kimetaka yeyote anayeweza kusaidia katika kukamatwa kwa mshukiwa kupiga ripoti kupitia nambari 0800 722 203.