Mike Sonko kupata Shahada ya Uzamifu (PhD) hivi karibuni

Muhtasari

•Sonko anadai kuwa alihitimu na shahada ya kwanza ya Utawala wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Methodist (KEMU) mnamo Julai 18, 2015.

•Amesema hivi karibuni atawaalika watu kwenye sherehe yake ya kuhitimu Phd.

Image: FACEBOOK// MIKE SONKO

Huku baadhi ya wanasiasa wenzake wakiendelea kuandamwa na masaibu kuhusiana na ustahiki wao wa kielimu kuwania nyadhifa mbalimbali, aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amedokeza kuwa anapanga kurudi katika chuo kikuu kupata Shahada ya Uzamifu (PhD).

Mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata mwingi amesema hivi karibuni huenda akawaalika watu kwenye sherehe yake ya kuhitimu Phd.

"Hivi karibuni nitawaalika kwa sherehe yangu ya kuhitimu PHD," Sonko alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Alikuwa anachangia kwenye mjadala mkubwa unaoendelea kuhusu ustahiki wa kielimu wa wanasiasa wanaogombea nyadhifa mbalimbali nchini.

Sonko alipakia picha kadhaa za kumbukumbu za sherehe yake ya kuhitimu iliyofanyika takriban miaka saba iliyopita.

"TBT..Mnajua mimi sikosi ushahidi ya kitu yoyote," Aliandika chini ya picha hizo.

Sonko anadai kuwa alihitimu na shahada ya kwanza ya Utawala wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Methodist (KEMU) mnamo Julai 18, 2015.

Picha ambazo mgombea huyo wa kiti cha ugavana Mombasa alipakia zinaonyesha kuwa naibu rais William Ruto ni miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla hiyo.

Azma ya baadhi ya wagombea iko katika hali ya mkanganyiko baada ya maswali kuibuliwa kuhusu ustahiki wao wa kielimu.

Baadhi ya wanasiasa ambao ustahiki wao umetiliwa shaka ni pamoja na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja na aliyekuwa CAS Wavinya Ndeti.

Sakaja anawania kiti cha ugavana wa Nairobi kwa tikiti ya chama cha UDA huku Wavinya akiwania ugavana wa Machakos.

Wapiga kura wawili wa Machakos wamewasilisha malalamishi katika tume ya uchaguzi wakipinga uhalali wa shahada ya Wavinya ya sayansi ya kompyuta kutoka chuo kikuu cha London. Wamehoji ni vipi Ndeti alifanikiwa kupata shahada ya Uzamili kabla ya shahada ya kwanza.

Sakaja pia anasubiri kujua hatima yake hukumu huku kesi inayopinga uhalisi wa shahada yake ya Shahada ya Sayansi katika Usimamizi kutoka Chuo Kikuu cha Timu cha Uganda ikitarajiwa kukamilika Jumapili.