Msichana wa shule atupwa nje ya matatu iliyokuwa inaendeshwa kasi Homabay

Muhtasari

•Mwanafunzi huyo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dudi iliyo kaunti ya Homa Bay alipata majeraha mabaya kutokana na tukio hilo .

•Alikimbizwa katika hospitali iliyo katika Kitongoji cha Rodi Kopany kabla ya kuhamishwa hadi Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay.

Hospitali ya Homa Bay County Teaching and Referral
Hospitali ya Homa Bay County Teaching and Referral
Image: ROBERT OMOLLO

Msichana wa shule ya upili alitupwa nje ya matatu iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi katika kile kinachodaiwa kuwa kisa cha wizi wa gari.

Mwanafunzi huyo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dudi iliyo kaunti ya Homa Bay alipata majeraha mabaya kutokana na tukio hilo la Jumanne jioni.

Jumatano, Chifu wa Kanyach Kachar Bernard Omuga alisema kisa hicho kilitokea baada ya abiria wawili wasiojulikana kuiba matatu katika kituo cha biashara cha Rodi Kopany huko Homa Bay.

Wahalifu hao wawili walijigeuza abiri na kuabiri gari lililokuwa likichukua abiria waliokuwa wakisafiri kuelekea Oyugis.

Mmoja wao alikaa kwenye kiti cha dereva mwenza na mwingine nyuma.

Wakati dereva na manamba waliposhuka kwenye gari kwa nia ya kuchukua abiria zaidi, mwanamume aliyekuwa kwenye kiti cha dereva mwenza alisogea kwenye kiti cha dereva na kuliendesha kwa mwendo wa kasi kuelekea mji wa Oyugis.

Hata hivyo gari hilo lilipofika katika kijiji cha Ndiru kando ya barabara ya Rodi Kopany – Oyugis, msichana huyo aliripotiwa kusukumwa nje wakati likiendeshwa kwa kasi.

"Msichana huyo atatuambia ukweli kwa sababu wengine wanasema msichana huyo alibingiria baada ya kusukumwa nje ya gari huku wengine wakisema aliruka nje ya gari baada ya kuhisi hatari," Omuga alisema.

Msichana huyo alikimbizwa katika hospitali iliyo katika Kitongoji cha Rodi Kopany kabla ya kuhamishwa hadi Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay.

Inaaripotiwa kuwa mhasiriwa alipata majeraha mabaya sehemu mbalimbali za mwili wake.

Abiria wengine hawajulikani walipo.

Omuga alisema washukiwa waliendesha gari hadi kusikojulikana.

"Mazungumzo yangu ya mwisho na manamba wa Rodi Kopany yalionyesha kuwa gari hilo bado halipo," alisema.

Afisa Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai  katika kaunti ndogo ya Homa Bay Monica Berege alisema wanachunguza kisa hicho.

Aliomba yeyote mwenye taarifa zaidi kuhusu tukio hilo na mahali walipo abiria hao afike kituoni ili kuharakisha upelelezi.

"Suala hilo halijaripotiwa kwetu lakini tunatafuta gari," Berege alisema.