Mshtuko baada ya bawabu wa shule kupatikana ameuawa Bungoma

Muhtasari

•Chifu Opicho alithibitisha kuwa bawabu huyo aliuawa Jumatano usiku na kusema alikuwa uti wa mgongo wa familia yake.

•Mwalimu mkuu alisema waliotekeleza mauaji hayo walifanikiwa kutoroka na vipatakilishi viwili pamoja na bidhaa zenye thamani isiyojulikana.

crime scene
crime scene

Hali ya mshangao ilitanda katika kata ndogo ya Milima, eneobunge la Tongaren, kaunti ya Bungoma  Alhamisi asubuhi baada ya bawabu wa shule ya upili ya Nabing’eng’e kupatikana ameuawa.

Chifu wa eneo hilo Martin Opicho alithibitisha mauaji hayo yaliyotekelezwa usiku wa Jumatano na kuyalaani vikali huku akimtaja marehemu kama mtu aliyejitolea kujenga jamii.

Opicho aliongezea kuwa bawabu huyo alikuwa uti wa mgongo wa familia yake na kusema ni jambo la kusikitisha kuwa aliuwawa kama kuku pasi na kuonyeshwa utu hata kiduchu.

“Aliyelala hapa alikuwa tegemeo Kubwa la familia yake na ni kinyume cha matarajio yetu kwamba aliuwawa bila ya utu wowote,” Chifu huyo alisema.

Bw. Opicho alisema kuwa aliarifiwa na wanakijiji kuhusu unyama huo alfajiri alipokuwa ametulia nyumbani kwake. Baada ya kupokea taarifa alikimbia katika eneo la tukio ambapo alikumbana na mwili wa marehemu ukiwa  umelala kwenye kidimbwi cha damu.

 “Nilipokea habari hizi mapema nikiwa bado nyumbani  na kukimbia moja kwa moja hadi pale nlipopata mwili wa mwendazake ukiwa amelala katika kidimbwi cha damu,’ alikariri Chifu huyo.

Kwa upande wake  mwalimu mkuu wa shule hiyo Frank Saisa alisema waliotekeleza mauaji hayo walifanikiwa kutoroka na vipatakilishi viwili pamoja na bidhaa zenye thamani isiyojulikana.

Mwalimu huyo aliyasema haya katika mahojiano ya moja kwa moja na wanahabari ambapo  alisema kuwa usimamizi wa shule hio umo mbioni kutambua aina na thamani ya vitu vilivyoibwa katika shambulizi la usiku huo.

“Mauaji ya bawabu huyu ni pigo Kubwa kwetu kama shule na jamii ya Nabing’eng’e kwa ujumla,” mwalimu huyo alisema.

Mwalimu huyo pia aliiomba idara ya usalama katika kanda hiyo kufanya uchunguzi wa kina na kuwafichua wahalifu hao.

Alisisitiza kuwa ni sharti wauaji hao watiwe mbaroni na kufikishwa mahakamani ili wajibu mashtaka yanayowakabili .

Kulingana na mwalimu huyo, mwili wa mwendazake uligunduliwa na baadhi ya wanafunzi waliofika shuleni kwa vipindi vya awali.

Wanafunzi hao walipiga  ripoti ambapo polisi kutoka Kimilili waliuchukua mwili wa marehemu na kuufikisha  kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha Kimilili huku familia ikianzisha mipango ya mazishi.

(Mhariri: Samuel Maina)