Wapelelezi wanamsaka mwanadada anayedaiwa kuwa mlanguzi sugu wa watoto

Muhtasari

•Elizabeth Emboyoga Litonde anaripotiwa kuwa nyuma ya ongezeko la visa vya kupotea kwa watoto wa shule.

•Yeyote aliye na taarifa zozote kuhusu mahali mshukiwa alipo ameombwa kuziwasilisha kwa wapelelezi.

Mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa mhusika katika biashara haramu ya ulanguzi wa watoto  anatafutwa na wapelelezi.

Elizabeth Emboyoga Litonde anaripotiwa kuwa nyuma ya ongezeko la visa vya kupotea kwa watoto wa shule hapa nchini Kenya.

Kitengo cha DCI kimeripoti kuwa baada ya kuwanyakua watoto hao, mshukiwa amekuwa akiwasafirisha hadi mataifa ya kigeni ambako wanatumika kama watumwa.

Litonde anaaminika kutorokea eneo la Magharibi mwa Kenya baada ya kugundua kuwa wapelelezi wanamsaka.

Yeyote aliye na taarifa zozote kuhusu mahali mshukiwa alipo ameombwa kuziwasilisha kwa wapelelezi.

"Taarifa zozote kuhusiana na alipo zitatusaidia sana kulinda maisha ya watoto wetu #FichuakwaCI 0800 722 203," Taarifa iliyotolewa na DCI Jumamosi ilisoma.

Idara hiyo ya upelelezi pia imeachia picha ya mshukiwa ili kusaidia wananchi katika utambuzi wa haraka.

Visa vya kupotea kwa watoto hasa wanaoenda shule vimekithiri hapa nchini katika miaka ya hivi majuzi.