Polisi ajeruhiwa vibaya baada ya wanadada wawili kuzozana juu yake Nairobi

Muhtasari

•Polisi huyo alipokuwa anabugia tembo yake alishirikisha mhudumu mmoja  kwenye mazungumzo ya kimapenzi. 

•Mueni aliweza kupata afueni lakini afya ya polisi huyo ikazorota mwendo wa saa tisa usiku wa kuamkia Jumapili na hapo akkimbizwa hospitalini.

Crime Scene

Polisi mmoja mwenye umri wa ujana anaendelea kupokea matibabu baada ya kujipata katika vita vilivyomhusisha yeye na wanawake wawili.

Afisa huyo anayehudumu katika kituo cha polisi cha Kware kilicho eneo la Embakasi, Nairobi alikuwa ameenda kukata maji katika baa ya kituo hicho wakati mzozo ulipochimbuka kati ya wanadada wawili waliokuwa wanamdai.

Kulingana na DCI, polisi huyo alipokuwa anabugia tembo yake alishirikisha mhudumu mmoja  kwenye mazungumzo ya kimapenzi. 

Mhudumu huyo aliyetambulishwa kama Mueni alionekana kuvutiwa na maneno matamu ya polisi huyo kwani baadae alisonga karibu naye na kukaa pale akitabasamu kwa furaha.

Sherehe za wawili hao hata hivyo zilikatizwa ghafla na mhudumu mwingine ambaye alionekana kutopendezwa na kilichokuwa kinaendelea.

Nekesa, kama alivyotambulishwa, ambaye alikuwa amewatazama wawili hao kwa muda alishindwa kuvumilia na kuenda kumkabili Mueni kwa ngumi na mateke.

Baada ya kumuangusha mhudumu huyo mwenzakekwa kishindo, Nekesa aliendelea kumshambulia polisi huyo kwa mtindo huo huo wa ngumi na mateke. Maafisa wengine waliokuwa karibu ndio waliokimbia katika eneo la tukio na kutenganisha vita hivyo.

Maafisa ambao walifika katika eneo la tukio walimkimbiza mwenzao na mpenzi huyo wake mpya katika kituo cha afya cha Mukuru ambapo walihudumiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani.

Mueni aliweza kupata afueni kikamilifu lakini afya ya polisi huyo ikazorota mwendo wa saa tisa usiku wa kuamkia Jumapili na hapo akkimbizwa hospitalini.

Kitengo cha DCI kimeripoti kuwa uchunguzi zaidi kuhusiana na kisa hicho unaendelea huku mhasiriwa akiendelea kupata afueni hospitalini. Afya yake hata hivyo tayari imeimarika.