Wanamgambo wa Al Shabaab wawapa msomo abiria kwa saa kadhaa Mandera

Muhtasari

• Kisa hicho kilitokea katika eneo la Dabacity, Kutulo, ambalo liko karibu na mpaka wa Kenya na Somalia siku ya Alhamisi.

• Maafisa wa usalama wanaosimamia vizuizi barabarani wameagizwa kutoruhusu watu wasio wenyeji kusafiri kwenye barabara kati ya Kotulo na Miji ya Elwak.

Magaidi wa Al-Shabaab walisimamisha basi na teksi na kuwapa msomo abiria waliokuwa ndani wakitafuta watu wasio wenyeji wa Kaunti ya Mandera. 

Kisa hicho kilitokea katika eneo la Dabacity, Kutulo, ambalo liko karibu na mpaka wa Kenya na Somalia siku ya Alhamisi.

Magari hayo yalisimamishwa katika eneo la Lag Barich kati ya Dabacity Town na Dimu Hill. Basi hilo lilikuwa likisafirisha abiria kutoka Nairobi kuelekea Mandera wakati wanamgambo hao waliokuwa na silaha nzito walipolisimamisha. 

Mashahidi walisema walikuwa wakitafuta watu wasio wenyeji. Waliamuru abiria wote washuke wakitafuta watu wasio wenyeji kwa zaidi ya saa mbili bila mafanikio. Pia walisimamisha teksi kutoka Kotulo iliyokuwa ikielekea Elwak na pikipiki iliyokuwa ikitoka Borehole 11 kuelekea kijiji cha Dimu. 

Baada ya kuwatafuta watu wasio wenyeji bila mafanikio, walitoa hotuba ndefu kwa lugha ya Kisomali ambayo wengi wa abiria hawakuielewa, baadhi ya abiria waliwaambia polisi. 

Mashuhuda hao walisema wakati huo baadhi wakiwapekua abiria hao, wengine walionekana kwenye vichaka kando ya barabara kuu ya B9. Hakuna aliyeumizwa katika basi hilo kwani hakukuwa na watu wasio wenyeji ndani ya basi.

Matukio kama haya siku za hapo nyuma yangeishia katika mauti. Mwezi Desemba 2019, abiria wanane ambao hawakuwa wenyeji waliuawa katika shambulio la wanamgambo katika eneo hilo hilo. Katika mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi ndani ya Kenya, al-Shabab mwaka wa 2014 waliteka nyara basi lililokuwa likisafiri kupitia Kaunti ya Mandera na kuwaua watu 28 wasio Waislamu. 

Maafisa wa usalama wanaosimamia vizuizi barabarani wameagizwa kutoruhusu watu wasio wenyeji kusafiri kwenye barabara kati ya Kotulo na Miji ya Elwak. Vikundi vya maafisa wa usalama vilitumwa katika eneo hilo kukabiliana na wanamgambo hao. 

Watu wenye silaha kali amabo pia wanaaminika kuwa sehemu ya wanamgambo hao walishambulia na kuharibu nguzo ya mawasiliano katika eneo la Slaughter, Rhamu, Kaunti ya Mandera na kuwaacha wengi bila uwezo wa kuwasiliana. 

Mkuu wa polisi kaskazini mashariki George Seda alisema wametuma maafisa zaidi wa polisi kuwafuata washambuliaji waliotoroka kuelekea mpakani. Hakuna jeraha lililoripotiwa katika tukio la hivi punde.  

Magaidi hao wamekuwa wakilenga vituo vya usalama katika eneo hilo. Hii ni licha ya kampeni za kukabiliana na tishio la ukosefu wa usalama katika eneo hilo.