Polisi walio likizoni waagizwa kurejea kazini ili kujitayarisha kwa ajili ya uchaguzi

Muhtasari

•Wale waliopanga kwenda likizo wameahirisha ili kuruhusu mipango ya kutosha ya uchaguzi wa Agosti.

•Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i amesema wako tayari kusaidia IEBC kufanya uchaguzi.

Mutyambai
IG Hillary Mutyambai Mutyambai

Maafisa wa polisi walio katika likizo wameagizwa kuripoti katika vituo vyao vya kazi kufikia Jumatatu ili kujitayarisha kwa uchaguzi.

Wale waliopanga kwenda likizo wameahirisha ili kuruhusu mipango ya kutosha ya uchaguzi wa Agosti.

Naibu Inspekta Jenerali wa polisi wa Kenya Edward Mbugua aliagiza wale walio kwenye likizo warudi kazini kufikia Julai 4.

“Kutokana na uchaguzi mkuu ujao, hakuna afisa yeyote anayepaswa kupewa likizo kuanzia Julai 1, 2022, isipokuwa kwa misingi ya matibabu na mapendekezo ya madaktari. Maafisa wote waliokuwa likizoni wataitwa tena na wawe kazini kufikia Julai 4, 2022,” alisema kwenye risala.

Maagizo kama hayo yatatumika kwa huduma zingine zote.

NPS inatazamiwa kutangaza katika gazeti la serikali makumi ya wafanyikazi wengine kutoka kitengo cha Magereza ya Kenya, Huduma ya Wanyamapori ya Kenya (KWS), Huduma ya Misitu ya Kenya na Huduma ya Kitaifa ya Vijana kama maafisa maalum ili kuimarisha usalama kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Polisi wamekuwa ikifanya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi ujao..

Maafisa kadhaa wamepewa mafunzo katika nyanja mbalimbali ili kushughulikia kwa ufanisi changamoto za usalama zinazojitokeza wakati wa uchaguzi.

Mwongozo unaoelezea miongozo kwa makamanda wa polisi wakati wa uchaguzi ujao ulizinduliwa mwezi Februari.

Mwongozo huo unaeleza kanuni za kutopendelea, kutendewa sawa, uwajibikaji na utawala wa sheria kwa maajenti wa usalama na unatoa taratibu za kudumisha utulivu wa umma wakati wa mchakato wa uchaguzi na njia za kutumika katika kuwasilisha malalamiko dhidi ya wafanyakazi wa usalama wa uchaguzi.

Inaeleza kwa kina njia za kuripoti makosa ya uchaguzi na inalenga kukamilisha kazi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka katika kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i amesema wako tayari kusaidia IEBC kufanya uchaguzi.

Polisi wanasema wameunda mkakati wa kina wa usalama na ujasusi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.

Aina fulani ya vurugu imeambatana na takriban kila uchaguzi katika historia ya Kenya, mtindo ambao mamlaka inataka kukomesha.

Maeneo yanayochukuliwa kuwa katika hatari ya vurugu yameorodheshwa na polisi watakuwa tayari kuepusha marudio ya 2007-08.

Baada ya matokeo ya urais ya uchaguzi mkuu wa 2007 kupingwa, ghasia zilizuka, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000. Wengine wengi walihamishwa.

Uchunguzi wa ghasia za baada ya uchaguzi ulionyesha kuwa polisi hawakuwa wamejitayarisha vyema, wenye msimamo mkali na wenye bidii katika kujaribu kutuliza ghasia hizo.

(Utafsiri: Samuel Maina)