Magoha awaonya wakuu wa shule dhidi ya kuwafukuza wanafunzi kwa kukosa karo

Waziri huyo aliahidi kuwa serikali itatuma pesa kwa mashule mwishoni mwa juma hii.

Muhtasari

•Magoha amewataka wazazi wanaoweza kumudu kulipa karo wafanye hivo ili wakuu wa shule na walimu wapate muda mwafaka wa kutekeleza majukumu yao shuleni.

•Masomo yataanza  leo kwa muhula wa pili, huku shule zikitarajiwa kuchukua mapumziko ya katikati ya muhula ifikapo Agosti 5 ili kupisha Uchaguzi Mkuu.

Waziri wa elimu George Magoha
Waziri wa elimu George Magoha
Image: MINISTRY OF EDUCATION

Waziri wa Elimu George Magoha amewaagiza wakuu wa shule kutowarudisha nyumbani wanafunzi ambao kufuatia deni la karo.

Jumatatu waziri huyo aliahidi kuwa serikali itatuma pesa kwa shule kufikia mwisho mwa juma hii.

“Nisisikie kuwa umemtuma mtoto kutoka shule ya Kenya arudi  nyumbani, Hilo halitakubalika,” alisema.

Hata hivyo, Magoha aliwataka wazazi ambao wanaweza kumudu kulipa karo wafanye hivo ili wakuu wa shule na walimu wapate muda mwafaka wa kutekeleza majukumu yao shuleni.

Aliyasema hayo jana katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kereri, kaunti ya Kisii ambapo aliongoza upanuzi wa awamu ya pili ya madarasa ya Mtaala unaozingatia Umahiri (CBC).

Kuhusu malalamishi ya walimu wakuu kwamba shule hizo zilitatizwa na bei ya juu ya bidhaa za kimsingi, Magoha alisema serikali inashughulikia mbinu za kupunguza bei ya mahindi.

"Nina uhakika kwamba ndani ya mwezi mmoja hivi serikali itakuwa imehakikisha bei ya mahindi inashuka," Magoha alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Kenya (KSSHA) Indimuli Kahi alikashifu gharama ya juu ya chakula akisema bei imeongezeka zaidi ya mara mbili katika wiki chache zilizopita.

"Hatuwezi kupunguza kiwango cha chakula ambacho watoto wamekuwa wakila kwa sababu tutakuwa tunajipiga risasi miguuni," Kahi alisema wakati wa mahojiano ya TV.

Masomo yataanza  leo kwa muhula wa pili, huku shule zikitarajiwa kuchukua mapumziko ya katikati ya muhula ifikapo Agosti 5 ili kupisha Uchaguzi Mkuu.