Lori la mafuta laanguka Thika Road

Njia mbili zilifungwa kufuatia ajali hiyo ambayo ilitokea Alhamisi asubuhi.

Muhtasari

•Njia mbili za barabara hiyo zilifungwa kufuatia ajali hiyo ambayo ilitokea Alhamisi mwendo wa asubuhi. 

•Polisi wanasafisha eneo la tukio kwa kutumia maji  huku magari ya kuelekea Nairobi yakielekezwa Githurai 44.

Ajali kati ya lori la mafuta na canter katika daraja la carwash, Roysambu.
Ajali kati ya lori la mafuta na canter katika daraja la carwash, Roysambu.
Image: HISANI

Usafiri katika sehemu ya Barabara kuu ya Thika umetatizaka baada ya lori la mafuta kupinduka katika daraja la Carwash lililo eneo la Roysambu, Nairobi.

Njia mbili za barabara hiyo zilifungwa kufuatia ajali hiyo ambayo ilitokea Alhamisi mwendo wa asubuhi. 

Msongamano mkubwa wa magari ulianza kushuhudiwa baada ya barabara hizo mbili za kuingia jijini Nairobi kufungwa.

Polisi wamewaelekeza madereva kutumia njia mbadala kwani mafuta yaliyomwagika yameifanya barabara kuwa na utelezi na kutokuwa salama kwa matumizi.

 Ajali hiyo pia imeathiri barabara ya Ruiru Bypass na barabara inayounganisha hadi Kasarani ambapo msongamano wa magari upo.

Polisi wanasafisha eneo la tukio kwa kutumia maji  huku magari ya kuelekea Nairobi yakielekezwa Githurai 44.

Hata hivyo hakuna watu walioonekana wakijaribu kuchota mafuta yaliyomwagika kama ilivyokuwa kawaida katika siku za awali.

Miaka ya hapo awali ajali zinazohusisha lori za mafuta zimewahi kusababisha maafa mengi baada ya umma kukimbia katika eneo la tukio katika juhudi za kuchota mafuta ya matumizi yao binafsi au ya kuuza.

Vifo pamoja na majeraha mengi yamewahi kushuhudiwa baada ya mafuta kugusana na moto.