Safaricom, Airtel na Telkom wazindua njia mpya za malipo kutumia simu

Mfumo huu wa malipo unatazamiwa kuwa salama, na wa haraka

Muhtasari

• Pendekezo hili pia linaambatana na kanuni za Mkakati wa Kitaifa wa Malipo, 2022 - 2025, uliozinduliwa na Benki Kuu ya Kenya mnamo Februari mwaka huu.

• Mkurugenzi mtendaji wa Safaricom alisema kuwa Ubunifu huo utatumika kwa kutuma pesa kutoka kwa huduma yoyote ya kifedha ndani ya nchi, na Kimataifa.

 

Wakurugenzi wa Kampuni ya Mawasiliano
Wakurugenzi wa Kampuni ya Mawasiliano
Image: HANDOUT

Wateja wa Airtel na Telkom sasa wanaweza kununua  na kulipia bidhaa kupitia simu moja kwa moja   kwenye nambari za Kulipa za M-PESA za Safaricom.

Hii itasaidia  Wakenya  sana haswa katika shughuli zao za  kibiashara  kwani wengi watakuwa huru kulipa na kupokea pesa.

Pendekezo hili pia linaambatana na kanuni za mkakati wa Kitaifa wa Malipo, 2022 - 2025, uliozinduliwa na Benki Kuu ya Kenya mwezi Februari mwaka huu.

Mfumo huu  wa malipo unatazamiwa kuwa salama, na wa haraka na utasaidia ujumuishaji wa kifedha utakao nufaisha Wakenya.

“Kutokana na ushirikiano na wateja wetu tumengundua  kwamba Wakenya wanathamini sana kutumia rununu kutuma pesa, kulipia bidhaa, kuweka akiba na  kukopa pesa, utapata huduma hii kwa kubonyeza  *160#.” Afisa mkurugenzi Mtendaji wa Telkom Kenya, Mugo Kibati alisema.

Kampuni  hizi za mawasiliano zilitoa tangazo hilo katika Shule ya Msingi ya Muguga Green, ambapo kila mmoja alilipa shilingi laki tatu kwenye nambari ya Malipo ya shule kutoka kwa pochi la pesa la kila mhudumu.

Pesa hizo, shilingi laki 9 za benki kuu ya Kenya zitatumiwa na shule hiyo kukidhi baadhi ya mahitaji yake kufadhili shughuli za muhula wa pili.

''Tunafurahi kuwa sehemu ya mabadiliko haya ambayo yanalenga kuwapa Wakenya mfumo wa malipo wa bei nafuu, unaofaa na salama, wateja wetu wanaweza kupata huduma hii kwa kubonyeza *222# au *334#.” Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Kenya, Ashish Malhotra alisema.

"Uzinduzi wa leo wa muingiliano wa namba ya Malipo kati ya M-PESA, Airtel Money na T-Kash, unafuatia ule wa 'Tuma Pesa  kwa kupitia nambari ya Tili,''Mkurugenzi Mtendaji wa Safaricom, Peter Ndegwa alisema.

Pia aliongezea kuwa Ubunifu huo utatumika kwa kutuma pesa kutoka kwa huduma yoyote ya kifedha ndani ya nchi na Kimataifa.