Jinsi polisi wawili wanavyodaiwa kutekeleza wizi wa bidhaa zenye thamani ya 600, 000

Lori lile lilipatikana likiwa limetupwa mbali huku bidhaa zote zilizokuwa ndani zikiwa zimetoweka

Muhtasari

•Sajenti John Lekidayo na Kontabo Kelvin Kinyua walikamatwa baada ya uchunguzi wa awali kuwahusisha na wizi uliofanyika Alhamisi.

•Dereva na wenzake walibebwa ndani ya Fielder kisha kuenda kutupwa karibu na soko la Kacibine, eneo la Imenti ya kati.

Mchoro wa afisa wa trafiki
Mchoro wa afisa wa trafiki
Image: The Star (Mchoro)

Maafisa wawili wa polisi wanazuiliwa na wapelelezi wa DCI katika eneo la Tharaka Kusini kwa madai ya wizi.

Sajenti John Lekidayo na Kontabo Kelvin Kinyua ambao wanahudumu katika kituo cha polisi cha Nkubu walikamatwa baada ya uchunguzi wa awali kuwahusisha na wizi  wa bidhaa zenye thamani ya shilingi laki sita uliofanyika Alhamisi.

Kulingana na ripoti ya DCI, wizi huo ulifanyika wakati Lori ambalo lilikuwa limebeba bidhaa za Hardware kutoka Isiolo kuelekea Tharaka Nithi lilisimamishwa na watu wanne waliodai kuwa maafisa wa polisi kwa madai kuwa  limebeba bidhaa haramu.

Maafisa hao walimtia pingu dereva Morris Nyaga pamoja na watu wawili wa kupanga mizigo, David Kuyo na Bonface Orito kisha kuwaweka ndani ya gari aina ya Toyota Fielder ambalo lilitumika kufungia lori hilo.

Watu wawili kati ya wanne waliodai kuwa polisi waliingia ndani ya lori baada ya dereva na wenzake kukamatwa.

Nyaga na wenzake walibebwa ndani ya Fielder hiyo kisha kuenda kutupwa karibu na soko la Kacibine, eneo la Imenti ya kati.

Baada ya hapo walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Kiagu na uchunguzi ukaanzishwa mara moja.

Baadae lori lile lilipatikana likiwa limetupwa mbali huku bidhaa zote  zilizokuwa ndani zikiwa zimetoweka.

Uchunguzi wa kina ulibaini kuwa gari lililotumika kutekekeleza wizi huo lilikuwa la sajenti Lekidayo. Pia ilibainika kuwa mnamo siku ya tukio Lekidayo alikuwa amemkabidhi Kinyua bunduki aina ya Ak-47 ambayo ilitumika katika wizi huo.

Mnamo siku ya tukio wawili hao walikuwa zamu katika sehemu ambayo haikuwa imeandikishwa kwenye kitabu cha zamu.

Washukiwa wanaendelea kuzuiliwa kituoni huku chunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo ukiendelea.