Ajali! Mbunge John Mbadi aponea katika ajali kaunti ya Siaya

Kulingana na picha gari hilo lilikuwa limegongwa vibaya upande wa kushoto.

Muhtasari

• Kioo cha pembeni pia hakikuwepo. Wakenya walijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kumtakia risala za heri njema. 

Gari la mbunge wa Suba Kusini John Mbadi lililopata ajali. Picha: JOHN MBADI/ FACEBOOK
Gari la mbunge wa Suba Kusini John Mbadi lililopata ajali. Picha: JOHN MBADI/ FACEBOOK

Mbunge wa Suba Kusini John Mbadi siku ya Jumatatu alinusurika kwenye ajali ya barabarani katika kaunti ya Siaya. 

Mbunge huyo alikuwa akirejea nyumbani kutoka kwa uzinduzi wa manifesto ya Seneta wa Siaya James Orengo ajali hiyo ilipotokea. Orengo anawania kiti cha ugavana. Mbadi alifichua kuwa kila mtu aliyekuwa ndani ya gari alitoka bila majeraha.

 "Asante, kwa kujali kwenu. Ingawa ilikuwa mbaya, nina furaha kusema kwamba mimi na wafanyakazi wangu tuliondoka eneo la tukio bila majeraha na tunamshukuru Mungu Mwenyezi," alisema.

 “Tunafarijiwa na maombi ya mtunga-zaburi kwamba, ‘Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya". 

Kulingana na picha gari hilo lilikuwa limegongwa vibaya upande wa kushoto. 

Kioo cha pembeni pia hakikuwepo. Wakenya walijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kumtakia risala za heri njema. 

"Aliye juu asifiwe kwa kuokoa maisha yako. Maisha yatakayotoa Homa bay na Kenya kwa ujumla" alisema Aben Janyidho. 

Calvince Odhiambo kwa upande wake alisema: “Mungu aendelee kukulinda, tunatoa shukrani nyingi kwake”. 

Mbadi aliweka kando azma yake ya kuwania ugavana wa kaunti ya Homa Bay na kutangaza kumuunga mkono Gladys Wanga na kujiunga na kamati ya kitaifa ya kampeni za Azimio.