Jamaa akiri kumbaka na kumuua mpenzi wa rafiki yake aliyekuwa amemfukuza kwake

Oduor alirejea nyumbani na kupata mwili wa mpenzi wake kitandani huku Tshirt ikiwa imeingizwa mdomoni

Muhtasari

•Odada anadaiwa kumvamia, kumbaka na kumnyonga mpenzi huyo wa rafikiye Samson Oduor katika mtaa wa Umoja kabla ya kumuua.

•Mshukiwa alikamatwa na wapelelezi kutoka kituo cha Dandora na hata kukiri kosa la kumuua mpenzi wa rafikiye.

•Mshukiwa wa pili, Samuel Juma Otieno, pia alitiwa mbaroni baada ya kupatikana na simu ya marehemu.

Mshukiwa Edwin Onditi Odada
Image: DCI

Polisi katika kaunti ya Nairobi wanamzuilia jamaa mmoja kwa madai ya kumuua mpenzi wa rafiki yake.

Edwin Onditi Odada alikamatwa Jumatano katika eneo la Kayole baada ya uchunguzi wa awali kubaini ndiye muuaji wa Pamela Asesa.

Odada anadaiwa kumvamia, kumbaka na kumnyonga mpenzi huyo wa rafikiye Samson Oduor katika mtaa wa Umoja kabla ya kumuua.

Kulingana na DCI, mnamo Julai 12 Oduor ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya uhandisi alirejea katika nyumba yake ya kukodi mwendo wa saa mbili usiku na kupata imefungwa.

Mwanzoni Oduor  alidhani kuwa mpenzi wake Asesa ambaye waliishi naye alikuwa ametoka kidogo

Dakika chache baadaye hata hivyo aliingiwa na shaka na kumpigia simu rafiki yake ambaye walivunja naye mlango kabla ya kukaribishwa na mshtuko mkubwa.

"Mwili wa Mchumba wake ambao haukuwa na uhai ulikuwa umelazwa juu ya kitanda chao. T-shirt ilikuwa imeingizwa mdomoni mwa marehemu, huku mwili ukiwa na alama za mikwaruzo kwenye shingo, kuashiria kuwa alinyongwa," Ripoti ya DCI inasoma.

Imeripotiwa kwamba mwili wa marehemu pia ulikuwa na ishara za unyanyasaji wa kingono kabla ya kuuawa.

Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa Odada ambaye ndiye mshukiwa mkuu alikuwa ameonekana akiondoka pale mwendo wa saa kumi alasiri.

Inaripotiwa kuwa Odada alikuwa akiishi kwa Oduor hapo awali kabla ya kufukwa. Oduor alimfukuza rafiki huyo wake aliyegeuka kuwa hasidi baada ya mkewe kumfahamisha kuwa alijaribu kumbaka.

Odour ambaye ni wazi alilenga kutimiza nia yake ya kumdhulumu Asesa alishambulia wakati mumewe akiwa kazini na kutekeleza unyama huo.

Mshukiwa alikamatwa na wapelelezi kutoka kituo cha Dandora na hata kukiri kosa la kumuua mpenzi wa rafikiye.

Mshukiwa wa pili, Samuel Juma Otieno, pia alitiwa mbaroni baada ya kupatikana na simu ya marehemu.

Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa Odada aliwahi kuhukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la unajisi ambalo alidaiwa kutekeleza mwaka wa 2017. Aliachiliwa mwaka wa 2020 baada ya kukata rufaa.

Washukiwa hao wawili wanazuiliwa katika kituo kimoja cha polisi jijini Nairobi kabla ya kufikishwa mahakamani.