Meta yaondoa maudhui hatari ya Kenya kabla ya uchaguzi

Meta pia imekataa matangazo 36,000 ya kisiasa kwa kutofuata sheria zake za uwazi.

Muhtasari

•Meta imeondoa maelfu ya machapisho yanayowalenga watumiaji wa Kenya kwenye Facebook kwa kukiuka sera zake kabla ya uchaguzi wa Agosti.

•Facebook inasema kuwa imeshirikiana na wakaguzi huru wa nchini Kenya kukanusha habari potofu kabla ya uchaguzi wa Agosti.

Image: BBC

Kampuni kubwa ya teknolojia ya Meta imeondoa maelfu ya machapisho yanayowalenga watumiaji wa Kenya kwenye mtandao wake wa kijamii wa Facebook kwa kukiuka sera zake kabla ya uchaguzi wa Agosti.

Miaka minne iliyopita, wakuu wa kampuni ya ushauri ya Cambridge Analytica inaonekana walinaswa kwenye kamera wakijivunia udhibiti walioutumia katika uchaguzi wa urais wa Kenya uliozozaniwa mwaka 2017, na kampuni yao ilishutumiwa kwa kuchimba data za binafsi za Wakenya kwenye Facebook kumsaidia Rais Uhuru Kenyatta kushinda.

Facebook sasa inasema katika ripoti mpya kwamba imeondoa machapisho zaidi 37,000 ya kueneza matamshi ya chuki na 42,000 kwa kukiuka sera zake dhidi ya uchochezi, katika muda wa miezi sita kabla ya tarehe 30 Aprili.

Kampuni hiyo pia inasema imekataa matangazo 36,000 ya kisiasa kwa kutofuata sheria zake za uwazi.

Facebook inasema kuwa imeshirikiana na wakaguzi huru wa nchini Kenya kukanusha habari potofu kabla ya uchaguzi wa Agosti.

Mkurugenzi wake wa sera za umma Mashariki na Pembe ya Afrika, Mercy Ndegwa, anasema wameimarisha udhibiti kwenye majukwaa yao ambayo yatarahisisha kutambua na kuondoa maudhui ambayo yanaweza kusababisha ghasia zinazohusiana na uchaguzi.