Mwanamke achoma mikono ya mabinti wake wawili kwa kula sukari

Wasichana hao wana umri wa miaka 6 na 8.

Muhtasari

•Mshukiwa anadaiwa kukasirika alipofika nyumbani na kugundua kuwa watoto walikuwa wamelamba sukari yake.

•Mwanamke huyo alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kinanie kabla ya kuhamishwa hadi Athi River.

Mmoja wa wasichana ambao mikono yao ilichomwa na mama yao kwa kulamba sukari huko Athi River, Kaunti ya Machakos mnamo Jumatano, Julai 20.
Mmoja wa wasichana ambao mikono yao ilichomwa na mama yao kwa kulamba sukari huko Athi River, Kaunti ya Machakos mnamo Jumatano, Julai 20.
Image: GEORGE OWITI

Mwanamke mmoja amekamatwa kwa kuchoma mikono ya binti zake wawili katika eneo la Athi River, Kaunti ya Machakos.

Chifu wa eneo la Kinanie, Josphat Isinga alisema mshukiwa alikamatwa baada ya kutekeleza unyama huo kwa kutumia kisu moto katika kituo cha kibiashara cha Kilili, eneo la Daystar mnamo Jumatano. Wasichana hao wana umri wa miaka 6 na 8.

"Mwanamke huyo anasemekana kuwachoma binti zake wa kuzaa baada ya kula sukari nyumbani kwake," Isinga alisema.

Isinga alizungumza kwenye simu siku ya Jumatano.

Alisema mwanamke huyo anayefanya kazi katika duka la chakula katika eneo la Kilili huko Kinanie alikasirika alipofika nyumbani na kugundua kuwa watoto wake walikuwa wamelamba sukari yake.

Chifu huyo alisema wazee wa kijiji waliitikia wito wa watoto hao baada ya mshukiwa kuwaumiz kwa moto.

Walipata majeraha mabaya kwenye mikono kabla ya kuokolewa na kukimbizwa katika hospitali ya Athi River Level 3 katika kaunti ndogo ya Mavoko.

Mwanamke huyo alikamatwa baadaye na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kinanie kabla ya kuhamishwa hadi kituo cha polisi cha Athi River.

Watoto hao waliokolewa na kuwekwa katika kituo cha uokoaji cha watoto ndani ya kaunti hiyo.

Isinga alisema mwanamke huyo atafikishwa mahakamani siku ya Alhamisi.