Wawili wakamatwa Umoja kwa kumuua mwanamke, kumtia nguo mdomoni

Mshukiwa mkuu alikuwa rafiki wa familia

Muhtasari

•Mshukiwa mkuu ameripotiwa kukiri kutekeleza mauaji hayo.

•Mshukiwa wa pili alipatikana akiwa na simu ya mkononi ya marehemu.

Crime
Crime Scene Crime
Image: HISSNI

Washukiwa wawili wakuu wametiwa nguvuni kuhusiana na mauaji ya ghafla ya mwanamke mwenye umri wa miaka 26 ambaye mwili wake ulipatikana katika nyumba yake huko Mowlem, Nairobi, na mdomo ukiwa umejaa vitambaa vya nguo.

Edwin Onditi Odada, mshukiwa mkuu wa mauaji ya Pamela Asesa mnamo Julai 12, ameripotiwa kukiri kutekeleza mauaji hayo.

Mshukiwa wa pili, Samuel Juma Otieno, alipatikana akiwa na simu ya rununu ya marehemu.

Rekodi za uhalifu zimefichua kuwa Odada hapo awali alihukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama Kuu ya Oyugis kufuatia kesi ya unajisi mwaka wa 2017.

Hata hivyo aliachiliwa baada ya kukata rufaa iliyofaulu mnamo 2020.

Wawili hao walikamatwa eneo la Tushauriane huko Kayole na wanashughulikiwa kwa ajili ya kufikishwa mahakamani, polisi walisema.

Pamela alikuwa amedai mshukiwa alijaribu kumbaka katika nyumba yao. Mshukiwa huyo alikuwa rafiki wa familia.

Mwili wake ulipatikana ndani ya nyumba yake ukiwa na majeraha shingoni na polisi wanasema alinyongwa.

Mdomo wake ulikuwa umejaa kipande cha nguo na kulikuwa na dalili za ubakaji kabla ya mauaji.

Uchunguzi wa polisi unaonyesha kuwa mpenzi wa marehemu alikuwa amerejea nyumbani kama kawaida mwendo wa saa nane usiku na kumpata amefariki.

Wawili hao walikuwa wakiishi pamoja katika nyumba ya kukodi katika eneo hilo.

Oduor, ambaye anafanya kazi katika kampuni ya uhandisi kando ya Barabara ya Mombasa, alifika nyumbani kwake na kupata mlango umefungwa.

Mwanzoni, alidhani kwamba huenda mchumba wake alikuwa ametoka kwenda kununua chakula cha jioni, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

Haikupita dakika zikageuka kuwa masaa bila yeye kujitokeza ndipo akahisi kuna kitu kisicho cha kawaida.

Aliwasiliana na rafiki ambaye alijitokeza mara moja na kwa pamoja, walivunja nyumba.

Humo walikuta mwili wake ukiwa umetapakaa kitandani kwao na nguo ikiwa imeingizwa mdomoni mwa marehemu.

Mkuu wa polisi wa Nairobi James Mugera alisema mshukiwa mkuu alionekana akitoka nyumbani kwa Oduor mwendo wa saa kumi jioni siku hiyo ya maafa.

Maafisa wa upelelezi wamebaini kuwa marehemu alikuwa ameripoti kwa mpenzi wake kwamba wakati mmoja katika tarehe ya awali, mshukiwa alijaribu kumbaka.

Mshukiwa huyo alikuwa marafiki wa karibu na Oduor na hata waliishi pamoja katika nyumba moja ambapo kitendo hicho cha kinyama kilifanyika.