Mwanamume ateketea hadi kufa ndani ya nyumba yake Nairobi

Familia zingine sita ziliachwa bila makao.

Muhtasari

•Mwanamume mwenye umri wa miaka 40 alifariki baada ya moto kuteketeza nyumba yake katika nyumba yake huko Makadara.

•Moto mwingine uliteketeza majengo katika mtaa wa California, Nairobi na kuacha takriban familia kumi bila makazi.

Moto mkubwa
Moto mkubwa
Image: WIKIPEDIA

Mwanamume mwenye umri wa miaka 40 alifariki baada ya moto kuteketeza nyumba yake katika nyumba yake huko Makadara, Nairobi.

Mwili wa Ochieng Ochibo ulipatikana muda mrefu baada ya moto huo kuzimwa.

Polisi na mashahidi walisema mwathiriwa alikuwa amelala wakati moto ulipozuka Jumanne asubuhi na kuteketeza majengo saba.

Familia zingine sita ziliachwa bila makao.

Mabaki ya mwili wa Ochieng’ yalihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti huku uchunguzi wa chanzo cha moto huo ukianzishwa, mkuu wa polisi wa Nairobi James Mugera alisema.

Alisema moto mwingine uliteketeza majengo katika mtaa wa California, Nairobi na kuacha takriban familia kumi bila makazi.

Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana. Polisi walisema hakuna majeruhi walioripotiwa lakini mali iliharibiwa katika kisa hicho cha moto.

Kukosekana kwa mwitikio wa kikosi cha zima moto mjini hapa kwa matukio ya aina hiyo kumekuwa kero kubwa kwa wengi.

Magari ya zima moto hayajawekewa bima jambo ambalo limesimamisha shughuli zao.

Maafisa katika Serikali ya Kaunti ya Nairobi wanasema wanafanya juhudi kutatua mzozo kati yao na kampuni ya bima.

Maeneo yaliyoathiriwa na matukio kama haya katika siku zilizopita yamekuwa yakitegemea vikosi vya moto vya kibinafsi kudhibiti. Baadhi ya watoa huduma hizo hudai malipo kwa huduma zinazotolewa.

Hili limeliweka jiji kwenye hatari nyingi iwapo kutatokea msiba.

Maafisa wanasema mazungumzo yanaendelea ili kushughulikia suala hilo.

Wakati huo huo, polisi wanawashikilia wanaume wanne kuhusiana na kupatikana kwa pikipiki nne ambazo zimeripotiwa kuwa zimeibwa.

Pikipiki hizo zilipatikana katika nyumba moja katika  mtaa wa mabanda wa Korogocho mnamo Jumanne katika operesheni ya polisi.

Pikipiki hizo nne zinazuiliwa kama vielelezo huku wanne hao wakitarajiwa kortini kujibu mashtaka mbalimbali, polisi walisema.

Polisi wamekuwa wakiwashauri wahudumu wa bodaboda kufunga vifuatiliaji kama sehemu ya juhudi za kukomesha visa vya wizi wa vifaa hivyo.

(Utafsiri: Samuel Maina)