Magoha aomba radhi husiana na matamshi dhalilishi dhidi ya mwanahabari

Magoha alimuuliza ripota wa kike aliyekuwa amevalia Hijab ikiwa alikuwa anawakilisha al-shabaab.

Muhtasari

• Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa shirika la NAMLEF Abdillahi Abdi, Magoha alikutana na mwandishi huyo pamoja na chama cha Waislamu na kuomba radhi.

 

Waziri wa Elimu George Magoha katika mkutano na viongozi wa Kiislamu Picha: FACEBOOK
Waziri wa Elimu George Magoha katika mkutano na viongozi wa Kiislamu Picha: FACEBOOK

Waziri wa Elimu George Magoha hatimaye ametii amri na kuomba msamaha kufuatia matamshi yake dhidi ya mwanahabari wa kike. 

Magoha amekuwa akishutumiwa kwa wiki moja iliyopita baada ya video yake akitoa matamshi yanayodhaniwa kuwa ya kudhalilisha wanawake wa Kiislamu kusambaa mitandaoni. 

Waziri huyo siku ya Alhamisi alikubali shinikizo na kuomba msamaha kwa matamshi hayo. Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa shirika la NAMLEF Abdillahi Abdi, Magoha alikutana na mwandishi huyo pamoja na chama cha Waislamu na kuomba radhi.

 "Waziri aliomba msamaha kwa mwandishi wa habari na kwetu sisi. Maneno yake yalikuwa 'unanihukumu na niko tayari kukubali uamuzi wako'," Abdi alisema. 

Abdi aliiomba jumuiya ya Waislamu pamoja na pande zote zilizoathirika kukubali msamaha wa Magoha. 

"Ninaamini msamaha huo ulikuwa wa kweli na ninaomba jamii ya Kiislamu kuukubali. Sisi viongozi tumekubali msamaha huo kwa niaba ya mwandishi wa habari na kwa niaba ya Umma," aliongeza. 

Katika video hiyo katika mitandaoni, Magoha alimuuliza ripota wa kike aliyekuwa amevalia Hijab ikiwa alikuwa anawakilisha kundi la al-shabaab. 

Mwandishi huyo wa habari alikuwa amemuuliza swali. 

“Unamwakilisha nani, ikiwa ni Al Shabaab sitakujibu...,” Magoha alisema. 

Baraza la vyombo vya Habari siku ya Jumatano lilidai kwamba Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano imlazimishe Magoha kuomba radhi kwa madai yake ya vitisho vya mara kwa mara dhidi ya wanahabari. 

Baraza hilo lilisema ni lazima Magoha awajibike ili kulinda heshima ya waandishi wanaomzungumzia yeye na wizara yake. 

"Baraza la vyombo vya habari linatoa wito kwa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano kuhakikisha waziri anaomba msamaha bila masharti, kuondoa matamshi ya kusikitisha, na kubatilisha agizo lake dhidi ya utendakazi mzuri wa vyombo vya habari," taarifa hiyo ilisema. 

Siku ya Alhamisi, FIDA-Kenya ilitishia kuwasilisha ombi kwa taasisi hiyo ikiwa Magoha atakataa kujiuzulu kutokana na matamshi yake. 

Ikiongozwa na mwenyekiti wake Nancy Ikinu, FIDA ilisema kwamba maneno ya Magoha yalikuwa ubaguzi na ukiukaji wa haki za binadamu.