(+Audio) Sauti ya anayedaiwa kuwa Junet akifanya mipango ya kuiba kura yavunjishwa

Anayedaiwa kuwa Junet anasikika akiomba afisa huyo kuandaa mkutano wa na maafisa wakuu wa IEBC.

Muhtasari

•Barasa ameachia audio ya mazungumzo yanayodaiwa kuwa kati ya Junet na afisa wa IEBC kuhusu mipango ya mkutano na makamishna wa tume ya uchaguzi na mipaka.

•Junet hata hivyo amejitokeza kupuuzilia mbali klipu hiyo ya sauti akisema ni ghushi.

JUNET.jfif
JUNET.jfif

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amemshtumu mwenzake wa Suna East Junet Mohammed kwa kupanga kuiba kura katika kinyang'anyiro cha Agosti 9.

Mwandani huyo wa naibu rais William Ruto ameachia audio ya mazungumzo yanayodaiwa kuwa kati ya Junet na mtu mwingine asiyetambulishwa kuhusu mipango ya mkutano na makamishna wa tume ya uchaguzi na mipaka.(IEBC)

Katika klipu hiyo, anayedaiwa kuwa Junet anasikika akiomba mwanaume huyo mwingine kuandaa mkutano wa ngazi ya juu na baadhi ya maafisa wakuu wa IEBC.

Mtu anayedai kuwa Junet anasikika akitoa agizo kwa mpokeaji simu kuwaleta mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, makamishna Abdi Guliye na Boya Molu na mkurugenzi mtendaji wa tume hiyo Marjan Hussein kwenye mkutano huo.

"Mh Junet Mohammed tunakufuatilia sana. Nitalihutubia taifa kesho saa kumi jioni nikiwa na maelezo na ushahidi wa majaribio yako ya kuvuruga uchaguzi. Hii itajumuisha mikutano ambayo umefanya na waandalizi wa kura za maoni  ili kumpendelea Raila Odinga. Ninataka kuwasalimu makamishna ambao wamekataa kuwa sehemu ya biashara hiyo ya tumbili," Barasa aliandika chini ya klipu hiyo ambayo alipakia Facebook.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko pia alishiriki klipu hiyo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Junet hata hivyo amejitokeza kupuuzilia mbali klipu hiyo ya sauti akisema ni ghushi.

"Rekodi ya sauti iliyokarabatiwa ambayo inazungushwa kwenye mitandao ya kijamiii ikidaiwa kumnasa Mhe. Junet Mohamed akizungumza na afisa wa IEBC ni FEKI," Junet alisema kupitia taarifa iliyofikia Radio Jambo.

Sikiliza audio iliyopakiwa na Barasa hapa:-

Mbunge huyo aliendelea kuwaomba Wakenya kupuuza sauti hiyo huku akialika vyombo vya uchunguzi kuchunguza suala hilo.

Alisema kuwa yuko bize kutika kampeni za kinara wa ODM Raila Odinga na kubainisha kuwa hana wakati wa kupanga njama ya kuvuruga uchaguzi.

"Ninawaomba umma kupuuza video hiyo, ambayo inaonekana kuwa moja ya vitendo vya mwisho vya kukata tamaa vya kampeni ya kisiasa inayokufa ambayo imekuwa ikiegemezwa kwa miaka mingi ya uwongo, uzushi, kupaka matop, kiburi, kujipiga kifua, kutaja majina, matus na sasa- kuamka kwa ukweli wa uchaguzi uliopotea- ni katika kutafuta huruma, "alisema .

Hali ya vuta nikuvute kati ya mirengo miwili pinzani , Kenya Kwanza na Azimio imeendelea kuchacha huku uchaguzi ukiwa umebakisha takriban siku kumi tu kufanyika.