Magoha anatazamia kuwa katika serikali mpya ili kusukuma mtaala wa CBC

Kuna zaidi ya wanafunzi milioni 1.2 ambao kwa sasa wako katika darasa la 6 na watajiunga na shule ya sekondari ya 'Junior'

Muhtasari

•Baadhi ya viongozi wanaoegemea muungano wa Kenya Kwanza pia wamekuwa wakikosoa Mtaala unaozingatia Umahiri (CBC)

•Magoha asema kuwa lazima amalize kazi ya ujenzi wamadarasa

Waziri wa Elimu George Magoha katika makao makuu ya KNEC wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCSE 2021 mnamo Aprili,23,2022.
Waziri wa Elimu George Magoha katika makao makuu ya KNEC wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCSE 2021 mnamo Aprili,23,2022.
Image: MERCY MUMO

Waziri wa Elimu Prof George Magoha mnamo Jumapili, Julai 31, aliisihi serikali ijayo kumruhusu muda zaidi kukamilisha ujenzi wa madarasa ya CBC.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa madarasa ya CBC katika Shule ya Sekondari ya Namgoi kaunti ya Nandi, Waziri huyo aliomba serikali mpya kufikiria kumpa muda zaidi kukamilisha mradi huo.

“Tunakusudia kumaliza ujenzi wa  madarasa ifikapo wakati wa uchaguzi, mimi si mwanasiasa, kitu najua unaweza kazi yangu, ni Mungu pekee ndiye anayejua nani atakuwa rais, sijui na yeyote atakayeingia, atakuwa kamanda wangu mkuu. Natumai kabla mtu huyo hajaingia aniruhusu nimalizie madarasa yaliyobaki,” Magoha alisema.

Kuna zaidi ya wanafunzi milioni 1.2 ambao kwa sasa wako katika darasa la 6 na watajiunga na shule ya sekondari ya 'Junior' mwaka ujao na serikali inashindana na wakati kuweka miundombinu sahihi ya kuruhusu mabadiliko ya haraka.

Waziri huyo aliwahakikishia walimu kwamba serikali imejitolea kuhakikisha kuwa madarasa yako tayari kabla ya mwisho wa mwaka huku shule ya upili ya 'Junior Secondary' ikianza Januari 2023.

Hata hivyo, mpeperushaji bendera wa Kenya Kwanza William Ruto ameelezea wasiwasi wake kuhusu CBC akibainisha kwamba mtaala huo unahitaji kupitiwa upya ili kushughulikia maswala kutoka kwa wazazi, walimu na washikadau wa elimu.

Baadhi ya viongozi wanaoegemea muungano wa Kenya Kwanza pia wamekuwa wakikosoa Mtaala unaozingatia Umahiri (CBC) kwa kutoa vitisho kwamba huenda utawala wa Ruto ukafutilia mbali mtaala huo mpya na kurejelea 8-4-4, ambao wanatazamia kutupa mbali.