Nancy Macharia awagiza wakurugenzi wa Elimu Kuwaachilia Walimu waliopewa kandarasi kama Maafisa wa Uchaguzi.

Aidha aliagiza wasimamizi wa taasisi kuhakikisha kuwa shule zote zilizoteuliwa na IEBC kama vituo vya kupigia kura zinapatikana kwa zoezi hilo.

Muhtasari

•Waziri Magoha hapo awali alidokeza kuwa taasisi hizo zitafungwa kuanzia Jumamosi lakini akaeleza kuwa uamuzi wa kuzifunga kuanzia Jumanne ulitokana na mashauriano zaidi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu Nancy Macharia
Image: ENOS TECHE

Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) Nancy Macharia amewaagiza Wakurugenzi wa Kaunti na Wakurugenzi wa Elimu wa Kaunti Ndogo kuwaachilia walimu waliopewa kandarasi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, kama maafisa wa uchaguzi.

Kupitia waraka wa Jumanne, Macharia aliwaagiza wakurugenzi wa elimu wa kaunti na kaunti ndogo kuhakikisha walimu wote wanaripoti shuleni mnamo Agosti 11, 2022, shule zitakapofunguliwa.

"Wapeni  ruhusa walimu wote ambao wamepewa kandarasi na IEBC kama maafisa wa uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu ujao ," Macharia alisema.

Aidha aliagiza wasimamizi wa taasisi kuhakikisha kuwa shule zote zilizoteuliwa na IEBC kama vituo vya kupigia kura zinapatikana kwa zoezi hilo.

Mnamo Jumanne, taasisi za elimu ya msingi ziliwaachilia wanafunzi kufuatia agizo la Waziri wa Elimu Magoha kwamba shule zifungwe kufikia Jumanne, Agosti 2, ili kuandaa njia kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Agosti 9.

Magoha kupitia taarifa kwa vyombo vya habari Jumatatu alisema kuwa shule zinapaswa kuwaachilia wanafunzi kwa mapumziko ya katikati ya muhula kwa muda wa siku kumi na kuanza tena Alhamisi tarehe 11 Agosti 2022.

Waziri Magoha hapo awali alidokeza kuwa taasisi hizo zitafungwa kuanzia Jumamosi lakini akaeleza kuwa uamuzi wa kuzifunga kuanzia Jumanne ulitokana na mashauriano zaidi.