Magoha aomba radhi kwa kufunga shule ghafla

Agizo la ghafla la kufunguwa kwa shule lilizua mdahalo mkubwa nchini

Muhtasari

• Magoha alisisitiza zaidi kwamba anazingatia ustawi wa watoto hasa katika kipindi hiki cha mpito.

Waziri wa Elimu George Magoha katika makao makuu ya KNEC wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCSE 2021 mnamo Aprili,23,2022.
Waziri wa Elimu George Magoha katika makao makuu ya KNEC wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCSE 2021 mnamo Aprili,23,2022.
Image: MERCY MUMO

Waziri wa Elimu Prof. George Magoha, ameomba radhi kwa niaba ya serikali kwa kufungwa kwa shule mapema. 

Akizungumza baada ya kuzindua madarasa mapya ya CBC katika shule ya upili ya Umoja mjini Eldoret, Magoha alisema hatua hiyo ni kuhakikisha maandalizi ya mapema ya uchaguzi unaofanyika Jumanne wiki ijayo. 

Magoha alisisitiza zaidi kwamba anazingatia ustawi wa watoto hasa katika kipindi hiki cha mpito. Siku ya Jumatatu, Magoha aliamuru shule zote zifungwe Jumanne, Agosti 2 na kwamba wanafunzi wataripoti Agosti 11. 

"Baada ya mashauriano, nawasilisha uamuzi wa Serikali kuhusu kufungwa mara moja kwa vyuo vyote vya elimu ya msingi kuanzia Jumanne, Agosti 2 hadi Jumatano, Agosti 10 ili kuhakikisha kuwa maandalizi na uendeshaji wa chaguzi zijazo unafanyika bila matatizo," CS Magoha alisema katika taarifa yake siku ya Jumatatu.  

Kulingana na ujumbe kutoka wizara ya elimu uamuzi huo uliafikiwa baada ya kufanyika kwa mashauriano baina ya idara mbali mbali za serikali.  

Hii ilikuwa kinyume na tangazo lake la awali, ambapo alisema shule zingefungwa Agosti 6  hadi Agosti 15 ili kupisha Uchaguzi Mkuu. 

Agizo la ghafla la kufunguwa kwa shule lilizua mdahalo mkubwa nchini huku wazazi wengi wakilalamikia hali ya kutojali kwa upande wa wizara ya elimu.