MCK:Tunashirikiana na wamiliki wa vyombo vya habari kuratibu matokeo

Omwoyo alikiri kuwa MCK imebaini wasiwasi unaoongezeka kuhusu matokeo tofauti yanayopeperushwa na vyombo tofauti vya habari.

Muhtasari

•Bosi huyo wa MCK alikumbusha hadhira kwamba matokeo rasmi yatatoka kwa tume huru ya uchaguzi na mipaka.

•MCK pia imeanzisha uchunguzi kuhusu kukamatwa na kuzuiliwa kwa ripota wa Pwani FM, Eric Munene

Mkurugenzi mkuu wa MCK, David Omwoyo
Image: MCK (Facebook)

Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya limesema linashirikiana na wamiliki wa vyombo vya habari na wahariri kutafuta njia ya kuratibu matokeo ya urais.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, afisa mkuu mtendaji wa MCK David Omwoyo alikiri kuwa shirika hilo limebaini wasiwasi unaoongezeka kuhusu matokeo tofauti yanayopeperushwa na vyombo tofauti vya habari.

“MCK iko katika mashauriano na wamiliki wa vyombo vya habari na wahariri kutafuta suluhu la dharura kwa hili ili kuhakikisha Wakenya wanapokea matokeo yaliyosawazishwa,” taarifa hiyo ilisema.

Omwoyo alisema kuwa siku za nyuma, vyombo vya habari vilifanya kazi pamoja katika masuala ya maslahi ya taifa kwa mafanikio.

Alisema matokeo yote yaliyopeperushwa, hata hivyo ni tofauti, yamejumlishwa kutoka kwa idadi iliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

Bosi huyo wa MCK alikumbusha hadhira kwamba matokeo rasmi yatatoka kwa tume huru ya uchaguzi na mipaka.

MCK pia imeanzisha uchunguzi kuhusu kukamatwa na kuzuiliwa kwa ripota wa Pwani FM, Eric Munene.

Munene, ambaye anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Likoni, anadaiwa kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu kuchelewa kwa masanduku ya kura katika kituo cha YMCA Likoni.

Polisi walisema wanahitaji maelezo zaidi kutoka kwake baada ya masanduku kutupwa na kuachwa katika eneo la kituo cha kujumlisha kura.