Washukiwa 3 wakamatwa baada ya viongozi wa Azimio kuwafumania na karatasi za kura

Polisi hata hivyo bado hawajatoa taarifa yoyote kuhusiana na suala hilo.

Muhtasari

•Viongozi wa Azimio walionekana wakimhoji mmoja wa washukiwa kuhusu karatasi walizodai kuwapata nazo.

•Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema karatasi zilizopatikana na washukiwa zilikuwa zaidi ya elfu moja.

Image: TWITTER// EDWIN SIFUNA

Polisi jijini Nairobi wanawazulia washukiwa watatu kwa madai ya kupanga njama ya kuiba kura.

Watatu hao walikamatwa katika eneo bunge la Starehe baada ya kufumaniwa na viongozi kadhaa wa Azimio wakiwa na karatasi za kura za viti mbalimbali.

Katika video iliyofikia Radio Jambo, baadhi ya viongozi wa Azimio walionekana wakimhoji mmoja wa washukiwa kuhusu karatasi walizodai kuwapata nazo.

Kulingana na CAS katika wizara ya Maendeleo ya Viwanda David Osiany, baadhi ya karatasi hizo zilikuwa zimewekwa alama huku zingine zikiwa wazi. Alisema karatasi hizo zilikuwa na mihuri ya IEBC.

"Tumekamata hitilafu huko Starehe. Karatasi za kupigia kura zisizo na alama na zilizotiwa alama mapema, bado zimegongwa muhuri. Kumbuka, karatasi zilipaswa kupigwa muhuri wakati wa utoaji. Bahati mbaya," Osiany alisema kupitia Facebook.

Viongozi waliofumania washukiwa ni pamoja na katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna, gavana wa Kitui anayeondoka Charity Ngilu, Mwakilishi wa Wanawake wa Nairobi Esther Passaris, Junet Mohammed, Rachel Shebesh miongoni mwa wengine.

Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema karatasi zilizopatikana na washukiwa zilikuwa zaidi ya elfu moja.

Alisema karatasi hizo za kura hizo zilipelekwa katika kituo cha polisi cha Central na kubainisha kuwa kesi hiyo inashughulikiwa.

"Lazima tuache kila kitu hapa na twende Bomas of Kenya ili IEBC ikomeshe haya," Ngilu alisema kwenye video hiyo.

Washukiwa wanazuilia katika kituo cha Central. Hata hivyo polisi bado hawajatoa taarifa yoyote kuhusiana na suala hilo.