Waziri Magoha apuuzilia mbali madai ya kuahirisha mitihani ya kitaifa

Mnamo Septemba 16, muhula wa pili utakamilika, na wanafunzi watakuwa na mapumziko ya wiki moja

Muhtasari

• Mwenyekiti wa muungano wa kitaifa wa wazazi Nicholas Maiyo, alikuwa amemtaka Magoha kuongeza muda wa shule kutokana na usumbufu uliosababishwa na uchaguzi wa Agosti 9.


Waziri wa Elimu George Magoha akihutubia wanahabari Kisumu mnamo Machi 21, 2022.
Waziri wa Elimu George Magoha akihutubia wanahabari Kisumu mnamo Machi 21, 2022.
Image: FAITH MATETE

Waziri wa elimu George Magoha,amekanusha madai ya kuharishwa kwa tarehe za mitihani ya kitaifa na kuongeza muda zaidi  wa muhula huu.

Magoha alisema kuwa mitihani ya kitaifa ya darasa la nane KCPE na ile ya kidato cha nne KCSE itafanywa jinsi ilivyoratibiwa kuanzia Novemba.

Aliongeza kuwa uchaguzi uliofanyika haukutatiza sana ratiba ya masomo hapa nchini,na haiwezi kuwa sababu kubwa ya kucheleweshwa kwa mitihani ya kitaifa.

"Watoto wetu ni werevu na wenye subira. Wengi wao walikuwa wamemaliza silabasi zao. Wana muda wa kutosha wa kufanya marudio na usalama wao ni muhimu,” Magoha alieleza.

Mwenyekiti wa muungano wa kitaifa wa wazazi Nicholas Maiyo, alikuwa amemtaka Magoha kuongeza muda wa shule kutokana na usumbufu uliosababishwa na uchaguzi wa Agosti 9.

Wazazi, kupitia kwa wawakilishi wao, pia walikuwa wametoa wito wa kupunguzwa kwa karo za shule ikiwa muda wa muhula huu hautaongezwa.

"Shule zilipaswa kufunguliwa Agosti 11, lakini ilisukumwa hadi Agosti 18. Ombi letu ni kwamba kalenda ya shule iongezwe au ikiwa haiwezekani, wapunguze karo," Maiyo alisema.

Mnamo Septemba 16, muhula wa pili utakamilika, na wanafunzi watakuwa na mapumziko ya wiki moja tu kabla ya kurejea kwa muhula wa tatu wa mwaka wa masomo wa 2022.