Azimio wawasilisha rufaa kwa njia ya kielektroniki

Mawakili hao wana hadi saa nane alasiri Jumatatu kuwasilisha rufaa ya kupinga ushindi wa Ruto.

Muhtasari

•Maanzo amethibitisha kuwa kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa rasmi kwa njia ya kielektroniki Jumatatu asubuhi katika Mahakama ya Juu.

•"Karatasi hizo zitawasilishwa Milimani kwa ajili ya kupigwa muhuri ili kuonyesha muda ambazo zimepokelewa." Maanzo alisema.

Mgombea urais wa Azimio Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua
Image: TWITTER// MARTHA KARUA

Timu ya wanasheria wa mgombea urais wa Azimio Raila Odinga tayari imewasilisha nakala ya kielektroniki ya rufaa kupinga ushindi wa Rais Mteule William Ruto.

Timu ya mawakili, kwa mujibu wa sheria, ina hadi saa nane alasiri Jumatatu kuwasilisha rufaa ya kupinga  ushindi wa Ruto.

Seneta mteule wa Makueni Dan Maanzo, mmoja wa mawakili katika timu ya wanasheria wa Azimio, amethibitisha kuwa kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa rasmi kwa njia ya kielektroniki Jumatatu asubuhi katika Mahakama ya Juu.

"Tayari tumewasilisha kesi mtandaoni inavyohitajika, maafisa wetu wanaofanya makaratasi watakuwa katika mahakama za Milimani wakati wowote," alisema Maanzo.

"Karatasi hizo zitawasilishwa Milimani kwa ajili ya kupigwa muhuri ili kuonyesha muda ambazo zimepokelewa."