Jinsi hali ya mlipuko wa homa wa nguruwe ilivyo Nakuru

Mtoto mmoja ameaga dunia kutokana na aina hii ya homa.

Muhtasari

•Idara ya afya katika kaunti hii imesajili takriban visa 140vya homa hii ingawa wanasema maambukizi yamedhibitiwa kwa sasa.

•Wakazi wa Nakuru wametakiwa kuchukua tahadhari ingawa serikali ya kaunti imetoa hakikisho kwamba ugonjwa huo hautaenea.

Image: HISANI

Kaunti ya Nakuru imeripoti mlipuko wa homa ya Nguruwe huku wizara ya afya ya kaunti hiyo ikirekodi visa zaidi ya 140.

Homa ya H1N1 imeenea kwa kasi katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.Mtoto mmoja ameaga dunia kutokana na aina hii ya homa.

Daktari Daniel Wainaina, afisa mkuu wa afya ya umma katika kaunti ya Nakuru anasema kuwa kisa cha kwanza kiliripotiwa katika kituo cha afya ya wadi ya Elementaita tarehe 27 mwezi wa July.

“Mwezi uliopita tarehe 27, tulipata ripoti kwamba katika eneo la Elementaita, zahanati ya Kitwangani kuna watoto walikuwa wanakuja wakiwa na homa kali na joto jingi mwilini,”Anasema Dkt Wainaina.

Aidha amesema kuwa maafisa wa afya walitumwa kuchunguza ni kipi kilikuwa kinatokea. Baadaa ya utafiti wa maabara ilibainika kwamba watoto hao walikuwa wakiugwa homa ya H1N1 ya Nguruwe.

Kufikia leo,idara ya afya katika kaunti hii imesajili visa zaidi ya 140 vya homa hii ingawa wanasema maambukizi yamedhibitiwa kwa sasa.

“Kufikia jana tumewaona wagonjwa mia moja na arubaini na kwa bahati mbaya mmoja wao ambaye ni mtoto wa chini ya mwaka mmoja aliaga dunia,” Anaeleza Bw Wainaina.

Wakazi wa Nakuru sasa wametakiwa kuchukua tahadhari ingawa serikali ya kaunti imetoa hakikisho kwamba ugonjwa huo hautaenea.

“Kwa wakati huu tuna watoto wananae katika wadi zetu.Sita wakiwa katika hospitali Kitongonyi na wawili katika hospitali kuu. Wanaendelea kupata matibabu na wakati wowote wataruhusiwa kuenda nyumbani,”Anasema daktari Daniel.

Afisa huyu anasema dalili ya homa hii ni joto jingi,Kikoozi, makamasi, maumivu ya kifua.