Barabara kadhaa kufungwa Nairobi Jumatatu huku mahakama ikitoa uamuzi wa kesi ya urais

Agizo la kufungwa kwa barabara litaanza kutekelezwa masaa mawili kabla ya wakati utakaotolewa na mahakama kuu

Muhtasari

•Huduma ya Polisi nchini imetangaza kuwa barabara ya Ngong itafungwa kwenye makutano ya Barabara ya Ngong 1st Avenue (mkabala na NHIF).

•Jumamosi polisi waliwashauri Wakenya kufuatilia kesi wakiwa nyumbani wakati Mahakama ya Upeo itakapokuwa ikitoa uamuzi wake.

Barabara
Image: MAKTABA

Barabara kadhaa jijini Nairobi zitafungwa siku ya Jumatatu huku Mahakama ya Upeo ikitarajiwa kutoa hukumu yake kuhusu kesi ya urais.

Katika taarifa, Huduma ya Polisi nchini imetangaza kuwa barabara ya Ngong itafungwa kwenye makutano ya Barabara ya Ngong 1st Avenue (mkabala na NHIF).

"Hakuna dereva atakayeruhusiwa kuingia CBD kupitia Kenyatta Avenue kupitia Cathedral Road lakini badala yake wanashauriwa kutumia Haile Selassie Avenue," Taarifa iliyotolewa na polisi Jumapili alasiri ilisema.

Barabara ya Cathedral/Milimani Ngong Road ambayo inapitia karibu na Mahakama ya Milimani pia itafungwa kwenye makutano ya Kenyatta Avenue/Valley Road (NSSF).

Magari ambayo yatakuwa yakielekea mahakamani ndiyo pekee yatakayoruhusiwa kutumia barabara hiyo. Madereva wengine wameshauriwa kutumia Valley Road.

Makutano ya Barabara ya Cathedral/ Haile Sellasie   yatafungwa na watumizi wa magari wanashauriwa kutumia njia mbadala ya Haile Sellasie/Ngong Road.

Agizo la kufungwa kwa barabara litaanza kutekelezwa masaa mawili kabla ya wakati utakaotolewa na mahakama kuu.

Siku ya Jumamosi polisi waliwashauri Wakenya kufuatilia kesi wakiwa nyumbani wakati Mahakama ya Upeo itakapokuwa ikitoa uamuzi wake.

Katika taarifa yake Jumamosi, kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Noor Gabow alishauri dhidi ya kukusanyika nje ya majengo ya mahakama katika mtaa wa Milimani, jijini Nairobi.

"Tunataka kushauri umma kwa ujumla kuepuka kukusanyika katika Mahakama ya Upeo wakati wa uamuzi, au kuwa katika mikusanyiko ya watu lakini wafuate kesi kutoka kwa starehe ya nyumba zao," Gabow alisema.

Aidha, kaimu Inspekta Jenerali alisema maeneo ya mahakama yatadhibitiwa kwa matumizi ya umma na barabara zote zinazoelekea katika Mahakama ya Upeo zitafungwa.

"Maafisa wa polisi wa trafiki watatumwa vya kutosha ili kuelekeza trafiki kuzunguka kituo cha mahakama," alisema.

Mahakama itatoa uamuzi wake kuhusu kesi hiyo Jumatatu, Septemba 5, 2022 baada ya kukamilika kwa kusikilizwa kwa siku tatu siku ya Ijumaa.