Hatimaye Uhuru ampongeza Ruto kwa kushinda uchaguzi na kumtakia heri njema

Uhuru alitangaza kwamba kesho siku ya Jumanne utawala wake wa awamu ya nne utafika tamati

Muhtasari

• Rais anaeondoka alichukuwa furasa hiyo kuangazia mafanikio ya serikali yake ya Jubilee tangu achukuwe madaraka mwaka 2013.

Rais Mteule William Ruto akisalimiana na rais anayeondoka Uhuru Kenyatta baada ya kukutana katika ikulu ya Nairobi. 12/9/2022
Rais Mteule William Ruto akisalimiana na rais anayeondoka Uhuru Kenyatta baada ya kukutana katika ikulu ya Nairobi. 12/9/2022
Image: PSCU

Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta siku ya Jumatatu kwa mara ya kwanza alimpongeza rais mteule William Ruto na kumtakia heri njema anapojiandaa kuchukuwa usukani kuliendesha taifa.

Uhuru alitangaza kwamba kesho siku ya Jumanne utawala wake wa awamu ya nne utafika tamati na kuashiria mwanzo wa utawala wa tano wake rais mteule William Ruto.

Uhuru ambaye alikuwa bado hajampongeza Ruto kwa kushinda uchaguzi wa Agosti 9, alisema atakuwepo katika uwanja wa Kasarani kumkabidhi Ruto rasmi ala za mamlaka.

Rais anaeondoka alichukuwa furasa hiyo kuangazia mafanikio ya serikali yake ya Jubilee tangu achukuwe madaraka mwaka 2013.

Uhuru alisema miongoni mwa maeneo waliyopata mafanikio makubwa ni pamoja na kulinda nchi dhidi ya mashambulizi ya kigaidi.

"Tulifanikisha hili kwa kurekebisha vyombo vyetu vya usalama na kuvifanya kuwa na uwezo zaidi wa kushughulikia changamoto za kisasa za usalama ambazo Kenya inakabili," Uhuru alisema.

Alizungumza katika Ikulu ya Nairobi, siku ya Jumatatu baada ya kufanya mkutano na Rais mteule William Ruto.

Uhuru aliendelea kusema kuwa utawala wa Jubilee hadi sasa umejenga kilomita 11,500 za barabara mpya zilizojengwa, na kuongeza mara mbili ya barabara zilizokuwepo wakati wakichukua serikali mwaka wa 2013.

Katika sekta ya kidijitali, Uhuru alisema utawala wake umeshuhudia ukuaji wa vituo vya televisheni kutoka 130 kutoka 14 mwaka 2013 na vituo 204 vya redio kutoka 130 mwaka 2013.

Pia alisema utawala wa Jubilee hadi sasa umeunganisha zaidi ya nyumba milioni 6.3 kwenye gridi ya umeme.