Gavana Otuoma aanzisha mikakati ya kustawisha Busia

Kaunti ya Busia imeshirikisha mashirika mbali mbali kufanikisha ajenda yake kwa wananchi.

Muhtasari

• Gavana Otuoma siku ya Jumanne alifanya mkutano na wawakilishi wa mashirika ya USAID, Wakfu wa Bill Gates, Britam, LapFund, Benki ya Dunia, na Unicef ​​kujadili mipango hiyo.

Gavana wa Busia Paul Otuoma
Gavana wa Busia Paul Otuoma

Serikali ya kaunti ya Busia imeshirikisha wataalam kutoka mashirika mbali mbali ya kimataifa kuwezesha ufanikishaji wa ajenda yake kwa wananchi.

Utawala wa gavana Paul Otuoma unataka kuwatumia wataalam hao kuweka msingi wa miradi ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa miji ya Busia na Malaba pamoja na uboreshaji wa huduma za afya.

Gavana Otuoma siku ya Jumanne alifanya mkutano na wawakilishi wa mashirika ya USAID, Wakfu wa Bill Gates, Britam, LapFund, Benki ya Dunia, na Unicef ​​kujadili mipango hiyo.

Wawakilishi wa mashirika hayo wakifanya kazi na maafisa wa kaunti, pia watatathmini mifumo ya mapato ya kaunti, michakato ya kutengeneza bajeti ili kuongeza mapato kwa wananchi, na kuunga mkono juhudi za kushirikisha umma kwa mipango ya maendeleo.

Mpango huo, gavana alisema, unalenga kuwahusisha wakaazi ili kupata njia bora za kushughulikia mambo ambayo utawala wa awali ushindwa kutekeleza.

Busia kwa miaka mingi - tangu kuanza kwa ugatuzi, imekuwa ikikejeliwa kutokana na miundombinu yake mibovu kutoka kituo kikuu cha mabasi, hospitali ya rufaa ya kaunti, na hali ya mabarabara.

Otuoma aliambia wanahabari baada ya mkutano huo kuwa wataalamu hao watapiga jeki mikakati ya serikali ya kaunti kubadilisha kufanikisha utekelezwaji wa manifesto yake.

“Baadhi wako tayari kusaidia katika ushirikishi wa umma na kuhakiki mpango wa maendeleo jumuishi wa kaunti. Tuko katika harakati za kufanya uhakiki wa tatu wa Mpango jumuishi wa Maendeleo ya Kaunti (CIDP) katika kaunti,” alisema.

Alisema mkutano wa Jumanne "ulijadili mipango iliyopo na inayohitajika kufanywa ili kuweka serikali kwenye msingi mzuri katika siku 100 zijazo."

Otuoma alisema majadiliano hayo yaliongozwa na mpango wa matokeo ya haraka (RRI)  uliochukuliwa na utawala wake kwa lengo la kustawisha mipango ya maendeleo ya muda mrefu ya serikali yake.

"Hii itahusu masuala ambayo kaunti inakabiliana nayo katika afya, miundombinu, sekta ya fedha, na usimamizi wa serikali ya kaunti ili kutoa huduma zinazofaa kwa wananchi," Otuoma alisema. 

Otuoma aliongeza kuwa wataalamu hao pia watasaidia kujenga uwezo wa mabunge ya kaunti kushughulikia masuala ya bajeti na sheria. 

“Mabunge ya kaunti yataundwa Aprili 22. Mojawapo ya ajenda kuu ni kushughulikia bajeti ya ziada.  Ili tuangalie bajeti za nyongeza, tunahitaji kuwahamasisha baadhi ya wahusika wakuu,” alisema. 

Kuhusu ushirikishwaji wa wananchi, gavana huyo alisema hatataka kuwe na mazingira ya kuanzisha miradi bila michango ya wananchi.

 "Wadau watatoa ushauri wa kitaalamu na kufadhili baadhi ya mipango kama vile ushirikishwaji wa umma kwenye mipango ya matokeo ya haraka kutoka ngazi ya vijiji hadi kata." 

Alitaja eneo la ICU katika hospitali ra rufaa ya Busia ambacho hakijafanya kazi kwa miaka miwili, mfumo wa kusafisha damu uliofeli, na kutokuwepo kwa bodi ya manispaa ya kusimamia miji katika kaunti hiyo kama baadhi ya masuala ambayo yanahitaji kukwamuliwa katika kaunti.

 "Ndio maana tunataka kuja na mtazamo kamili kwa baadhi ya masuala ili tunapoanza kuyatekeleza, kumekuwa na ushirikishwaji wa umma, yamefikiriwa vyema," Otuoma alisema.