Kwa nini AG anafaa kuwa na wasiwasi kuhusu uteuzi wa majaji sita - Mutula

Gavana Mutula anasema AG Kihara Kariuki anafaa kuwajibikia jukumu lake katika kutoteuliwa kwa majaji 6 na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.

Muhtasari

• Gavana huyo anasema AG alipinga uteuzi wa majaji hao licha ya agizo la mahakama lililoelekeza Rais kuwaapisha majaji hao. 

Gavana mteule Mutula
Gavana mteule Mutula
Image: Hisani

Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Junior sasa anasema Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki anafaa kuwajibikia jukumu lake katika kutoteuliwa kwa majaji sita na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta. 

Gavana huyo anasema AG alipinga uteuzi wa majaji hao licha ya agizo la mahakama lililoelekeza Rais kuwaapisha majaji hao. 

"Mwanasheria mkuu anapaswa kuwa na wasiwasi. Alipinga uteuzi wa Majaji licha ya maagizo ya wazi ya mahakama na nafasi yake kama mwanachama wa JSC. Hatua zake kuhusu suala hili hazifai kuachwa bila kushughulikiwa," Kilonzo alisema. 

Rais William Ruto siku ya Jumanne aliwateua majaji sita mara tu baada ya kuapishwa kama Rais wa tano wa Kenya. 

Hao ni majaji wa rufaa Weldon Korir, George Odunga, Aggrey Muchelule na Joel Ngugi, Evans Makori na Judith Omange wa Mahakama ya Mazingira. 

Majaji hao walikuwa miongoni mwa wengine 40 walioteuliwa mwaka 2019 baada ya zoezi kali la kuhakikiwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kati ya Julai na Agosti mwaka huo huo. Mnamo Juni 2021, Uhuru aliteua majaji 34 lakini akawaacha nje majaji sita akitaja masuala ya uadilifu. 

Mnamo Oktoba 2021 punde tu baada ya Mahakama Kuu kuamuru Uhuru kuteua majaji waliosalia ndani ya siku 14, Kariuki alikata rufaa dhidi ya uamuzi huo. AG alisema hakuridhishwa na agizo la mahakama kama ilivyotolewa na majaji James Wakiaga, William Musyoka na George Dulu. 

Jopo la majaji watatu lilisema katika uamuzi wao kwamba Rais anaweza kutengwa katika mchakato wa kuwateua majaji.Mnamo Oktoba 1, 2021, Mahakama ya Rufaa ilisimamisha kwa muda agizo lao.