Waiguru achaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Magavana

Naibu wake atakuwa Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi.

Muhtasari

•Waiguru alichaguliwa Jumamosi, baada ya kikao cha uzinduzi cha magavana na manaaibu gavana mjini Mombasa.

•Waiguru alipendekezwa na Muungano wa Kenya Kwanza kushindana na gavana wa Kajiado wa Azimio Joseph Ole Lenku.

Gavana wa Kirinyaga Annne Waiguru
Image: MAKTABA

Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Magavana.

Yeye ndiye mwenyekiti wa kwanza mwanamke wa baraza hilo na atachukua nafasi ya aliyekuwa Gavana wa Embu Martin Wambora.

Waiguru alichaguliwa Jumamosi, baada ya kikao cha uzinduzi cha magavana na manaaibu gavana mjini Mombasa.

Naibu wake atakuwa Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi.

Gavana wa Nandi Stephen Sang ndiye kinara wa baraza la magavana.

Waiguru alipendekezwa na Muungano wa Kenya Kwanza kushindana na gavana wa Kajiado wa Azimio Joseph Ole Lenku.

Sekretarieti ya Baraza la Magavana ilisema Waiguru alichaguliwa kupitia maafikiano.

"Tungependa kuthibitisha mchakato wa kuchagua uongozi wa kitaifa wa Baraza la Magavana ulikuwa mzuri. Magavana wote walikubali kupitia maelewano kuhusu uongozi mpya," afisa mkuu mtendaji wa CoG Mary Mwiti alisema.

Awali Waiguru alihudumu kama naibu mwenyekiti wa kwanza wa Baraza hilo mwanamke kuanzia Desemba 2017 hadi Januari 2019.

Viongozi hao watatu walizinduliwa Jumamosi alasiri katika hafla iliyopambwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula.

Wetangula alimwakilisha Rais William Ruto, ambaye alitarajiwa kufunga rasmi kikao hicho cha siku tatu.

Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa atakuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, naye Kenneth Lusaka wa Bungoma atasimamia Kilimo.

Gavana wa Taita Taveta Andrew Mwadime ametwikwa jukumu la kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Maji na gavana wa Kisumu Anyang Nyongo atasimamia Ardhi.

Nafasi ya mwenyekiti wa CoG iliundwa na Sheria ya Mahusiano ya Kiserikali ya 2012 ili kusimamia shughuli za magavana.

Viongozi kadhaa wamejitokeza kumpongeza, huku Gavana wa Embu Cecily Mbarire akiongoza.