Nick Mwendwa achukua usukani tena katika afisi za FKF

Mwendwa amejitokeza na kuchukua udhibiti wa ofisi za shirikisho hilo katika Goal Project.

Muhtasari

•Mwendwa aliingia katika majengo ya FKF mapema Jumanne akiandamana na afisa mkuu mtendaji Barry Otieno na maafisa wengine wengi.

•Utawala unaoongozwa na Mwendwa ulitimuliwa ofisini Novemba mwaka jana na waziri wa Michezo Amina Mohamed

Rais wa FKF Nick Mwendwa
Image: MAKTABA

Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa amejitokeza na kuchukua udhibiti wa ofisi za shirikisho hilo katika Goal Project huko Kasarani.

Mwendwa aliingia katika majengo ya FKF mapema Jumanne akiandamana na afisa mkuu mtendaji Barry Otieno na maafisa wengine wengi.

Haya yanajiri wiki moja tu baada ya kutoa dokezo la hila kuwa alikuwa akipanga kuchukua tena usimamizi wa soka humu nchini.

Utawala unaoongozwa na Mwendwa ulitimuliwa ofisini Novemba mwaka jana na waziri wa Michezo Amina Mohamed ambaye baadaye aliunda kamati ya muda ya kuendesha soka nchini.

Waziri huyo alisema uamuzi wake ulitokana na madai mazito ya ufisadi yanayokabili afisi hiyo iliyofukuzwa.

Uamuzi huo wa Amina ulipelekea Kenya kufungiwa kushiriki michuano ya kimataifa na shirikisho la soka duniani, FIFA.

FIFA ilidai kurejeshwa kwa Mwendwa kama sharti la kuondoa marufuku hiyo.

Mnamo Septemba 8, Mwendwa alizua taharuki alipomwandikia barua Rais wa Fifa, Gianni Infantino, akieleza nia yake ya kutaka kurudisha uongozi wa FKF.