Wakulima kununua mbolea ya bei nafuu katika bohari za NCPB

"Kila mkulima mmoja atastahili hadi magunia 100 ya kilo 50," alisema Owino.

Muhtasari

•Owino alisema katika taarifa yake kwamba mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya DAP utauzwa kwa Sh3,500, CAN Sh2,875, urea Sh3,500, NPK Sh3,275, MOP kwa Sh1,775 na Sulphate ya Ammonia Sh2, 220.

Wakulima wakusanya mbolea ya ruzuku katika bohari ya NCPB mjini Eldoret mnamo Juni 13
MBOLEA ILIYOBORESHWA: Wakulima wakusanya mbolea ya ruzuku katika bohari ya NCPB mjini Eldoret mnamo Juni 13
Image: MATHEWS NDANYI

Wakulima sasa wanaweza kununua mbolea katika bohari za karibu za bodi ya nafaka (NCPB), hii ni kulingana na katibu mkuu katika Wizara ya Kilimo Francis Owino.

Owino alisema katika taarifa yake kwamba mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya DAP utauzwa kwa Sh3,500, CAN Sh2,875, urea Sh3,500, NPK Sh3,275, MOP kwa Sh1,775 na Sulphate ya Ammonia Sh2, 220.

"Ili kuhakikisha uwasilishaji mzuri na njia za udhibiti zimewekwa, mbolea itapatikana kupitia bohari kubwa na ndogo za Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao [NCPB] nchini kote, kuanzia Septemba 19, 2022.

"Kila mkulima mmoja atastahili hadi magunia 100 ya kilo 50," alisema PS.

Owino alisema mbolea hiyo ya ruzuku itasaidia kilimo cha takriban ekari milioni 1.4 za ardhi.

Rais William Ruto alikuwa ameagiza kwamba mbolea iuzwe kwa Sh3,500 kwa kila gunia la 50Kg kutoka Sh6,500.