Miili ya polisi waliouawa Turkana yasafirishwa hadi Nairobi

Polisi wanane, chifu mmoja pamoja na mwanamke mmoja waliuawa katika shambulizi hilo.

Muhtasari

•Miili ya polisi waliouawa Jumamosi katika shambulio la majambazi huko Turkana Mashariki iliwasili Nairobi Jumapili jioni.

•Mwanamke aliyeuawa katika shambulizi hilo ni dadake kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance Ekuru Aukot.

Ambulensi iliyobeba miili ya maafisa wa polisi waliouawa kwenye shambulizi la majambazi Turkana ikiondoka Uwanja wa Ndege wa Wilson, Nairobi, ilipowasili kwa chopa ya polisi mnamo Septemba 25.
Ambulensi iliyobeba miili ya maafisa wa polisi waliouawa kwenye shambulizi la majambazi Turkana ikiondoka Ambulensi iliyobeba miili ya maafisa wa polisi waliouawa kwenye shambulizi la majambazi Turkana ikiondoka Uwanja wa Ndege wa Wilson, Nairobi, ilipowasili kwa chopa ya polisi mnamo Septemba 25.
Image: ANDREW KASUKU

Miili ya maafisa wa polisi waliouawa Jumamosi katika shambulio la majambazi huko Turkana Mashariki iliwasili Nairobi Jumapili jioni.

Miili hiyo ilisafirishwa kwa chopa ya polisi hadi Uwanja wa Ndege wa Wilson na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Forces Memorial, Nairobi.

Maafisa wanane wa polisi, chifu mmoja pamoja na mwanamke mmoja waliuawa katika shambulizi hilo lililotekelezwa na watu wanaoshukiwa kuwa ni majambazi wa Pokot.

Waathiriwa walivamiwa walipokuwa wakifuatilia genge la majambazi waliokuwa wamejihami vikali wanaoshukiwa kutoka katika kaunti jirani ya Baringo.

Kamanda wa Polisi wa Turkana Samuel Ndanyi alithibitisha kisa hicho akisema waathiriwa waliviziwa katika eneo la Namariat karibu na kijiji cha Kakiteitei.

Alisema watu wanaoshukiwa kuwa majambazi wa Pokot walitoka eneo la Tiaty kaunti ya Baringo.

Msafara wa usalama ulijumuisha maafisa wa GSU, NPRs na maafisa wa majukumu jumla.

Walikuwa wakiwafuata majambazi waliokuwa wamejihami vikali ambao walikuwa wamevamia kijiji cha Ngikengoi katika eneo ndogo la Elelea, wadi ya Katilia na kuiba mifugo.

Mwanamke aliyeuawa katika shambulizi hilo ni aliyekuwa afisa mtendaji wa kaunti ya Samburu Mary Kanyaman, dadake kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance Ekuru Aukot.

Alikuwa akiwaongoza maafisa hao kurejesha mifugo iliyoibiwa ya babake.