UDA yakanusha madai ya kuongeza muda wa urais

Alifafanua kuwa Mbunge wa Fafi Salah Yakub hakuwa akizungumza kwa niaba ya chama.

Muhtasari
  • Kupitia kwa mwenyekiti wa chama hicho Johnson Muthama, UDA ilisema wanasalia kuunga mkono mchujo wa sasa wa miaka 10
Mwenyekiti wa UDA Johnson Muthama wakati wa mkutano na wanahabari katika ofisi yake ya Gigiri siku ya Jumatatu.
Mwenyekiti wa UDA Johnson Muthama wakati wa mkutano na wanahabari katika ofisi yake ya Gigiri siku ya Jumatatu.
Image: MERCY MUMO

Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kimejitokeza kukashifu madai kwamba chama hicho kinataka kuongeza mihula ya urais.

Kupitia kwa mwenyekiti wa chama hicho Johnson Muthama, UDA ilisema wanasalia kuunga mkono mchujo wa sasa wa miaka 10.

Muthama alisema amepokea simu nyingi huku kukiwa na taharuki kuhusu suala hilo.

"Kauli ya Mbunge wa Fafi, Mhe. Salah Yakub kuhusu kufutilia mbali ukomo wa muhula wa urais na kuweka kikomo cha umri imewafanya Wakenya wengi kuwa na wasiwasi na wengi wamenipigia simu wakitaka nafasi ya UDA Kenya," Muthama alisema.

Alifafanua kuwa Mbunge wa Fafi Salah Yakub hakuwa akizungumza kwa niaba ya chama.

"Tafadhali zingatia hili, kama Chama cha Kitaifa, Mwenyekiti ningependa kutamka wazi kwamba Mhe. Yakub alitoa tamko la kibinafsi ambalo halihusiani na UDA Kenya," Muthama aliongeza.

Yakub katika pendekezo lake anadai chama kinapaswa kuwa kinazingatia umri na sio huduma ya muda.

Mbunge huyo wa Fafi alisema baadhi ya wabunge wa UDA kwa sasa wanafanyia kazi mswada wa marekebisho ya Katiba ili kubadilisha ukomo wa mihula miwili na ukomo wa umri wa miaka 75.

Yakub alifichua mpango huo wakati wa harakati ya kusambaza chakula cha msaada huko Garissa mwishoni mwa juma.