Ruto amjibu Raila kwa kuwatetea makamishna 4 wa IEBC

Rais alimkashifu Raila akisema naibu mwenyekiti wa IEBC Julian Cherera na wenzake watatu lazima wawajibishwe.

Muhtasari

• Raila alisema kuwa Ruto ana nia ya kuweka kibaraka wake katika  IEBC kwa kumtimua Cherera na makamishna hao watatu.

RAIS WILLIAM RUTO
Image: PCS

Rais Wiliam Ruto amemjibu Kinara wa Azimio Raila Odinga kuhusu utetezi wake dhidi ya makamishna wanne wa IEBC wanaokabiliwa na tishio la kubanduliwa afisini.

Rais alimkashifu Raila akisema naibu mwenyekiti wa IEBC Julian Cherera na wenzake watatu lazima wawajibishwe kwa kujaribu kubatilisha maamuzi ya kidemokrasia ya wananchi.

Raila siku ya Alhamisi alimshutumu Ruto kwa kurudisha nchi katika enzi za udikteta wa Nyayo akisema ataongoza shinikizo kupinga hilo.

"Mabwana wa ukiukaji sheria, ambao waliharibu taasisi za uangalizi kwa kutumia udanganyifu wa handshak, wanapaswa kuruhusu bunge kuwashughulikia maafisa walaghai wanaoweka taifa hatarini kwa kuhujumu matakwa ya kidemokrasia ya wananchi kuwajibika," Ruto aliandika kwenywe Twiter.

Ruto alisema Bunge linafaa kuruhusiwa kuendelea na uchunguzi wake kuhusu mienendo ya makamishna hao wanne "walaghai".

Makamishna hao ni Juliana Cherera naibu mwenyekiti, Francis Wanderi, Justus Nyang'aya na Irene Masit.

Kinara wa upinzani Raila siku ya Alhamisi alikuwa amewataka makamishna hao wanne kususia vikao vya bunge kwa "maslahi ya uzingatiaji wa katiba na sheria".

Alidai kuwa Ruto alikuwa katika harakati za kulipiza kisasi dhidi ya makamishna hao wanne aliowataja kuwa wazalendo kwa kumpinga Mwenyekiti wao Wafula Chebukati.

wakati wa mkutano uliopita na wanahabari katika hoteli ya Serena.
Makamishna wa IEBC Justus Nyangaya, makamu mwenyekiti Juliana Cherera, Irene Masit na Francis Wanderi wakati wa mkutano uliopita na wanahabari katika hoteli ya Serena.
Image: REUTERS

Raila alisema kuwa Ruto ana nia ya kuweka kibaraka wake katika  IEBC kwa kumtimua Cherera na makamishna hao watatu.

Raila alisema kwa kuwaita makamishna hao, Bunge linanyakua jukumu la mahakama.

 “Ni mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati pekee ndiye aliyepatikana kufanya kazi upande mmoja, tatizo hili kwa hivyo limechochewa kisiasa na ni mwendelezo wa juhudi za Ruto kuwadhulumu watu ambao anahisi sio vibaraka wake,” alisema Raila.