Moses Kuria awapa wakulima saa 72 kutoa mahindi yaliyohifadhiwa

Aliwataka wakulima katika eneo la Bonde la Ufa kukoma kuhifadhi mahindi.

Muhtasari
  • Akitetea GMO, alikariri kuwa utawala wa Kenya Kwanza uliondoa marufuku hiyo ili kuwasaidia wananchi waliokuwa na njaa
  • Kuria alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa Wakenya hawafi na njaa, wala si kudhuru mapato ya wakulima

Waziri wa Biashara Moses Kuria amesema ikiwa wakulima hawatatoa mahindi yaliyohifadhiwa, serikali italazimika kuagiza kutoka nje.

Alisema wana saa 72 za kuleta mahindi kwenye hifadhi yao, kufikia Jumanne.

Iwapo kufikia wakati watakuwa hawajazingatia agizo hilo, baraza la mawaziri linaweza kulazimishwa kuruhusu uingizaji wa mahindi kutoka nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya mazishi ya mwanahabari Evelyn Ogutu mjini Kitale siku ya Jumamosi, Kuria alisema baraza la mawaziri litakutana Jumanne ili kuamua jinsi ya kusonga mbele.

Aliwataka wakulima katika eneo la Bonde la Ufa kukoma kuhifadhi mahindi.

"Mkitoa mahindi mimi najua mambo itakuwa sawa. Tunaelekea mwezi ya tatu na tutaendelea kuomba mvua imyeshe."

Alisema serikali inajitahidi kupunguza bei ya  mbolea na kuongeza kuwa itawakomboa wakulima endapo watalazimika kuuza mahindi kwa Sh4,000 kwa gunia.

"Najua kuna suala la msingi. Vinginevyo tutaelezeaje kuagiza mahindi kutoka Argentina ili kuyauza kwa bei nafuu kuliko yanayozalishwa nchini," alisema.

"Hiyo ndiyo hadithi ninayotaka tuijadili. Najua inahusiana na samadi na miche."

Akitetea GMO, alikariri kuwa utawala wa Kenya Kwanza uliondoa marufuku hiyo ili kuwasaidia wananchi waliokuwa na njaa.

Kuria alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa Wakenya hawafi na njaa, wala si kudhuru mapato ya wakulima.

"Hii stori ya GMO ni mada ambayo nisingependa tuizungumzie, niwaambie, bei ya unga wa mahindi ikishuka hadi Sh120, hutanisikia tena nikizungumzia vyakula vilivyobadilishwa vinasaba." alisema.