Naibu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera ajiuzulu

Cherera alimwandikia barua rais William Ruto na kumfahamisha kuhusu kujiuzulu kwake.

Muhtasari

•Katika barua yake kwa rais William Ruto, Cherera alimjulisha kuhusu kujiuzulu kwake kutoka kwa baraza hilo la  uchaguzi.

•Haya yanajiri baada ya  kamishna wa IEBC, Justus Nyang'aya kujiuzulu kutoka wadhifa wake Ijumaa wiki iliyopita.

Makamishna wa IEBC Justus Nyangaya, makamu mwenyekiti Juliana Cherera, Irene Masit na Francis Wanderi
Image: REUTERS

Naibu mwenyekiti wa tume ya IEBC Juliana Cherera amejiuzulu kwenye wadhifa wake katika tume hiyo.

Katika barua yake kwa rais William Ruto, Cherera alimjulisha kuhusu kujiuzulu kwake kutoka kwa baraza hilo la  uchaguzi.

"Ni kwa masikitiko makubwa kwamba leo ninawasilisha ombi langu la kujiuzulu kama kamishna na naibu mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka," barua hiyo ilisoma.

Cherera alisema katika kipindi chake kama kamishna alitekeleza majukumu yake kwa bidii, umakini na kuweka juhudi za dhati katika kuisaidia tume kushughulikia masuala ya utawala bora katika mazingira magumu sana.

"Kama naibu mwenyekiti, siku zote nilitetea haki na fursa sawa kwa wafanyakazi wote," alisema.

Hata hivyo, naibu mwenyekiti huyo wa zamani alibainisha kuwa matendo yake wakati wa uchaguzi ambayo alifanya kwa nia njema, kwa bahati mbaya yalihukumiwa na kutafsiriwa vibaya.

Baada ya kutafakari kwa kina matukio ya sasa katika tume hiyo na kushauriana na familia yake na mawakili, Cherera alisema kwamba alikubali kukaa kwake katika tume hiyo hakustahili tena na hivyo akachagua kujiuzulu.

"Ninamshukuru kwa dhati Mheshimiwa William Samoei Ruto, Rais wa Kenya kwa nafasi niliyopewa ya kutumikia jamhuri, Mungu akubariki," alisema.

Haya yanajiri baada ya  kamishna wa IEBC, Justus Nyang'aya kujiuzulu kutoka wadhifa wake Ijumaa wiki iliyopita.

"Ni kwa moyo mzito kwamba ninawasilisha kujiuzulu kwangu kama kamishna wa IEBC kuanzia leo (Ijumaa)," Nyang'aya alisema katika barua kwa Rais William Ruto.

Nyanga'aya na makamishna wengine watatu wanatuhumiwa kwa kujaribu kubadilisha matakwa ya wananchi katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9.

Wengine wawili ni Kamishna Irene Masit na Francis Wanderi.

Matokeo manne yalikanushwa ambayo yalitangazwa na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.