Raila asisitiza ushindi wake uliibiwa, aahidi kufichua kilichotokea

Raila alisisitiza kuwa wanajua kilichofanyika na wako tayari kumwaga mtama hivi karibuni.

Muhtasari

•Raila amesisitiza kuwa mkutano wa kuipinga serikali kati yake na wafuasi wake uliopangwa kufanyika baadaye wiki hii utaendelea.

•Raila alidokeza kuwa kulikuwa na wizi katika uchaguzi wa urais uliofanyika takriban miezi minne iliyopita. 

Odinga azungumzia Wahindi waliotoweka
Odinga azungumzia Wahindi waliotoweka
Image: HISANI

Kiongozi wa ODM Raila Odinga ameendelea kuchukua nafasi yake ya upinzani kwa nguvu zote na kukosoa utawala wa Kenya Kwanza.

Raila ambaye alipoteza azma yake ya urais kwa mara ya tano kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, amesisitiza kuwa mkutano wa kuipinga serikali kati yake na wafuasi wake uliopangwa kufanyika baadaye wiki hii utaendelea.

"Mkutano wetu wa Jumatano ijayo utaendelea kama ilivyopangwa. Tukutane Kamukunji," Raila alitangaza kwa wafuasi wake kupitia ukurasa wake wa Twitter Jumapili jioni.

Kiongozi huyo wa Azimio- One Kenya alitoa tangazo hilo baada ya kufanya mkutano wa hadhara katika mtaa wa Utawala, Nairobi ambapo aliwasihi wafuasi wake kujitokeza kwa wingi katika  mkutano huo wa Jumatano.

Raila vilevile alidokeza kuwa kulikuwa na wizi katika uchaguzi wa urais uliofanyika takriban miezi minne iliyopita. Alisisitiza kuwa upande wake unajua kilichojiri na wako tayari kumwaga mtama hivi karibuni.

"Tunajua walifanya nini, jinsi walivyofanya na ni nani aliyewasaidia kuifanya. Tutafichua hayo yote hivi karibuni," alisema.

Huku akiwahutubia wafuasi wake katika mtaa wa Utawala siku ya Jumapili, Raila alimshutumu rais William Ruto kwa kuwafuta kazi makatibu wakuu kwa madai ya kutengeneza nafasi ya kuwaajiri watu wake.

Alisema makatibu wakuu ni watumishi wa umma na bila kujali utawala unaounda serikali, hawapaswi kuondolewa ofisini.

“Makatibu wakuu ni watumishi wa umma ambao hawatakiani ati serikali ikibadilika wanafutwa kazi,” alisema.

"Amefuta principal secretaries karibu wote, halafu yeye analeta ubaguzi. Hawa watu wote ameleta ni kabila lake."

Raila anatazamiwa kukutana na wafuasi wake katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi mnamo Desemba 7 na Desemba 12 ambapo anatarajiwa kufichua hatua yake ifuatayo. Hapo awali, rais Ruto aliwaomba upinzani kutoa ratiba ya maandamano yao ili mipango ya kuhakikisha usalama wao ifanyike.