3 wakamatwa kwa mauaji ya chifu wa Laikipia, Kindiki azuru eneo la uhalifu

Silaha inayoaminika kutumika katika mauaji ya chifu huyo mkuu wikendi ilipatikana.

Muhtasari

•Kindiki alisema msako wa kuwatafuta wahusika zaidi katika mauaji ya Jacob Loyangile wa lokesheni ya Il Motiok, eneo bunge la Laikipia Kaskazini unaendelea.

•Chifu huyo aliuawa na majambazi waliokuwa wamejihami kwa kupigwa risasi katika boma lake mnamo Desemba 4, Jumapili jioni.

Pingu
Image: Radio Jambo

Washukiwa watatu wamekamatwa na kupatikana na silaha inayoaminika kutumika katika mauaji ya chifu mkuu katika kaunti ya Laikipia wikendi.

Waziri wa Mambo ya Ndani Prof. Kithure Kindiki alisema msako wa kuwatafuta wahusika zaidi katika mauaji ya Jacob Loyangile wa lokesheni ya Il Motiok, eneo bunge la Laikipia Kaskazini unaendelea.

Kambi ya polisi inayosimamiwa na Kitengo cha GSU, Rapid Deployment Unit, na Kitengo cha Kupambana na Wizi wa Mifugo itazinduliwa mara moja katika eneo hilo ili kuimarisha ulinzi.

Akizungumza katika kijiji cha Tiamamut baada ya kuwaongoza maafisa wakuu wa usalama katika kufariji familia ya marehemu chifu, Waziri huyo aliapa kwamba mauaji hayo hayatapita bila kuadhibiwa.

“Tunapogawana mzigo wa huzuni na familia ya Mzee Loyangile na kuwasilisha rambirambi zetu kwa watu wa Laikipia Kaskazini, muwe na uhakika kwamba hakuna hata mmoja wa wahalifu hawa atakayekwepa haki. Wakati wao umefika sasa,” alisema.

Chifu huyo ambaye alikuwa amebakisha mwezi mmoja pekee kustaafu aliuawa na majambazi waliokuwa wamejihami kwa kupigwa risasi katika boma lake mnamo Desemba 4, Jumapili jioni.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba alilengwa kimakusudi kutokana na uwazi wake dhidi ya kulazimishwa kwa wakazi katika eneo hilo kuhama na majambazi kutoka kaunti jirani.

Kindiki aliwahakikishia wakazi hao ulinzi dhidi ya kufukuzwa kwa lazima akisema serikali italinda haki yao ya kumiliki na kuishi katika maeneo yao kama haki ya Kikatiba.

“Kila Mkenya ana haki ya kuishi na kumiliki mali popote pale, na tutatumia nguvu zetu zote kulinda haki hii. Mmechagua viongozi wenu na kuweka serikali yenye uwezo. Pia unalipa kodi ili kulindwa kutokana na uhalifu huo wa kifidhuli, na tutafanya hivyo kwa gharama yoyote ile,” alisema.

Waziri huyo alitangaza kuajiri askari zaidi wa Kitaifa wa Akiba wakiwemo 360 ambao wataanza mafunzo yao Jumatatu.

Watasaidia timu za mashinani kutekeleza usalama na kuimarisha vita dhidi ya wizi wa mifugo, ujambazi na uhalifu wa jumla.

Kindiki, ambaye aliandamana na Inspekta Jenerali Japheth Koome na Mkuu wa Mkoa wa Bonde la Ufa Maalim Mohammed, pia alisema wafanyikazi wa ziada kutoka vitengo maalum watatumwa katika eneo hilo.