Wanafunzi 252 walioshikwa wakiiba mtihani kujiunga na shule za upili

Wanafunzi husika watapokea matokeo lakini watapewa sufuri katika somo ambalo walidanganya.

Muhtasari

•Hatua hii inaambatana na sera ya serikali ya kuhakikisha kuwa asilimia 100 ya wanafunzi wanaofanya mtihani wa darasa la nane wanajiunga na shule za upili.

Waziri wa elimu Ezekiel Machogu akitangaza matokeo ya KCPE 2022, siku ya Jumatano 21.12,2022.
Waziri wa elimu Ezekiel Machogu akitangaza matokeo ya KCPE 2022, siku ya Jumatano 21.12,2022.
Image: ANDREW KASUKU

Idadi ya wanafunzi walionaswa wakidanganya kwenye mtihani wa KCPE wa mwaka huu imepungua ikilinganishwa na mwaka uliyopita.

Akitangaza matokeo ya mtihani wa mwaka huu wa KCPE siku ya Jumatano, Waziri wa elimu Ezekiel Machogu alisema kwamba ni wanafunzi 252 pekee waliopatikana na hatia ya udanganyifu wa mtihani wa KCPE mwaka huu.

Waziri Machogu hata hivyo alitangaza kuwa wanafunzi hao hawataachwa nje na wataruhusiwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Kulingana na Machogu hatua hii inaambatana na sera ya serikali ya kuhakikisha kuwa asilimia 100 ya wanafunzi wanaofanya mtihani wa darasa la nane wanajiunga na shule za upili.

Kinyume na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo wanafunzi waliodanganya katika mtihani wa KCPE hawakupokea matokeo yao, mwaka huu wanafunzi hao watapokea matokeo lakini watapewa sufuri katika somo ambalo walishikwa wakidanganya.

Jumla ya wanafunzi 1,244, 188 walifanya mtihani wa KCPE mwaka huu uliyofanywa kati ya Novemba 28 na Novemba 30.

Ukitaka kupata matokeo ya mwanafunzi tuma nambari yake ya mtihani kwa 20076, ujumbe utatozwa shilingi 25.

Pia, walimu wakuu wa shule husika wanaweza kupakua na kuuchapisha matokeo ya wanafunzi wa shule zao kutoka kwa tovuti ya baraza la mitihani (www.knec-portal.ac.ke).