Watahiniwa wa KCPE 2022 kujua shule za upili watakazojiunga nazo leo Jumatatu

Waziri Machogu ataongoza kuachiliwa kwa upangaji wa wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza.

Muhtasari

•Takriban watahiniwa 1,233,852 walifanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane mwaka jana na matokeo yao kutangazwa mnamo Desemba 21, 2022.

•Waziri Machogu alitangaza kuwa wanafunzi wote ambao walipokea matokeo yao wangejiunga na shule ya upili.

Waziri wa elimu Ezekiel Machogu akitangaza matokeo ya KCPE 2022, siku ya Jumatano 21.12,2022.
Waziri wa elimu Ezekiel Machogu akitangaza matokeo ya KCPE 2022, siku ya Jumatano 21.12,2022.
Image: ANDREW KASUKU

Watahiniwa wa KCPE 2022 ambao walipokea matokeo yao mwezi uliopita watapata kujua shule ya upili ambazo wamechaguliwa kujiunga nazo baadae siku ya Jumatatu, Januari 16.

Takriban watahiniwa 1,233,852 walifanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane mwaka jana na matokeo yao kutangazwa mnamo Desemba 21, 2022.

Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu, anatarajiwa kuongoza kuachiliwa kwa upangaji wa wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza katika shule za upili mbalimbali  kwa mwaka 2023 katika Taasisi a Kukuza Mtaala ya Kenya (KICD).

Wakati akitangaza matokeo ya KCPE 2022 wiki chache zilizopita, waziri Machogu alitangaza kuwa wanafunzi wote ambao walipokea matokeo yao wangejiunga na shule ya upili.

Machogu alisema wanafunzi ambao walinaswa wakidanganya pia hawataachwa nje na wataruhusiwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Alifichua kwamba ni wanafunzi 252 pekee waliopatikana na hatia ya udanganyifu wa mtihani wa KCPE mwaka uliopita.

Kulingana na Machogu hatua hii inaambatana na sera ya serikali ya kuhakikisha kuwa asilimia 100 ya wanafunzi wanaofanya mtihani wa darasa la nane wanajiunga na shule za upili.

Kinyume na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo wanafunzi waliodanganya katika mtihani wa KCPE hawakupokea matokeo yao, mwaka huu wanafunzi hao watapokea matokeo lakini watapewa sufuri katika somo ambalo walishikwa wakidanganya.