Gachagua atoa maagizo kwa Magavana kuhusu utoaji leseni kwa baa

Alidokeza kuwa vijana ndio walioathirika zaidi kwani walikuwa wakipata pombe siku nzima.

Muhtasari
  • Kwa upande wake, Rais Willian Ruto alidokeza kuwa wasimamizi wa serikali ya kitaifa watafanya kazi pamoja na serikali za kaunti kukabiliana na wale wanaouza pombe haramu
Image: Twitter

Naibu Rais Rigathi Gachagua alitoa wito kwa magavana wote kukagua utoaji wa leseni za baa na mikahawa katika kaunti ambazo alibaini zilikuwa na mapungufu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Nyumba za Nafuu katika Kaunti ya Kiambu mnamo Alhamisi, Januari 18, Gachagua alibainisha kuwa vitengo vilivyogatuliwa vilikuwa na sehemu nyingi za burudani ambazo zilikuwa zimefunguliwa kwa saa 24.

Alidokeza kuwa vijana ndio walioathirika zaidi kwani walikuwa wakipata pombe siku nzima.

"Tunataka kutoa wito kwa magavana wetu kuketi na kukubaliana kwamba hawawezi kutoa leseni kwa kila baa na mkahawa kuuza kwa saa 24. Ni makosa," alisema.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Nyumba za bei nafuu huko Ruiru, Kaunti ya Kiambu, Gachagua alisema eneo hilo linapoteza kizazi kizima kutokana na ulevi.

"Mnaweka kila bar kukua bar and restaurant mkitafuta revenue at the expense of our children, in the process we lose an entire generation."

Kwa upande wake, Rais Willian Ruto alidokeza kuwa wasimamizi wa serikali ya kitaifa watafanya kazi pamoja na serikali za kaunti kukabiliana na wale wanaouza pombe haramu.

"Lazima tuhakikishe hatuwatoi watoto wetu kafara kwa gharama ya pesa. Tutashirikiana katika hilo," alisema.

Utoaji wa leseni za baa umejadiliwa katika wiki za hivi majuzi, haswa, kaunti ya Nairobi ambapo Gavana Johnson Sakaja aliamuru kufungwa kwa sehemu za burudani katika maeneo ya makazi.

Alibainisha kuwa familia nyingi zimeathirika wakati wa usiku kutokana na kelele.